HUKU kumbukumbu za tukio la uvamizi wa kigaidi
lililosababisha mauaji ya wanafunzi 147 wa Chuo Kikuu cha Garissa nchini
Kenya zikiwa bado hazijafifia vichwani, hali ya ulinzi Chuo Kikuu Cha
Dar es Salaam ‘Mlimani’ inasababisha mguno kutokana na watu kupita ndani
ya chuo hicho bila ukaguzi.
Kwa
mujibu wa taarifa zilizokifikia kitengo maalum cha Oparesheni Fichua
Maovu ‘OFM’ cha Global Publishers, pamoja na chuo hicho kuweka walinzi
kwenye mageti yake mawili (Ardhi na Maji), lakini ukaguzi kwa wenye
magari binafsi na ya umma haufanyiki jambo ambalo limetajwa kuwa, kama
magaidi wakitokea wanaweza kupenya chuoni hapo.
“Kama unavyojua ulinzi wetu nchini mpaka
jambo litokee ndiyo unaimarishwa, ndiyo ilivyo hata pale UDSM. Ukaguzi
hakuna, mtu anaweza kuingia na mzigo wowote akiwa kwenye gari binafsi na
akapita zake tu getini.
“Sasa
wewe chukulia ndiyo magaidi wanaingia pale chuo kama wenzetu kule Kenya
si itakuwa kazi rahisi sana! Hatuombei itokee lakini wajitahidi
kukagua, nyie njooni mjionee ili muwakumbushe wahusika, msiishie huko
mitaani,” alisema mwanafunzi mmoja akiomba jina lake lisitajwe.
Kama
ilivyo kawaida, Jumatatu iliyopita, OFM ilitinga chuoni hapo kwa
usafiri wake ambapo ilishuhudia magari binafsi na ya umma yakipita
getini huku walinzi wakiwa wamesimama na mara kadhaa kuelekeza madereva
bila kukagua.
Hata
magari ambayo pengine yangepaswa kutiliwa shaka, mfano yenye vioo vya
giza ‘tinted’ au binafsi ambayo hubeba watu wengi na yale ya mizigo
yalikuwa yakipita eneo hilo bila ukaguzi japokuwa kuna kibao nje ya geti
kinachosema kwa lugha mbili: TAFADHALI SIMAMA ONYESHA ULICHONACHO/
PLEASE STOP DECLARE YOUR PERSONAL EFFECTS.
Ili
kuthibitisha udhaifu huo, OFM ikiwa na gari lake ilipita mbele ya
walinzi hao kuanzia geti la Chuo cha Ardhi mpaka kwenda kutokea upande
wa Maji bila kizuizi.
Baada ya hapo, OFM iligeuza kurudi na
kwenda Kituo Kidogo cha Polisi Mlimani ili kuzungumza na uongozi kuhusu
hali ya ulinzi ambapo ilielezwa mwenye mamlaka ya kusema ni afisa
uhusiano wa chuo ambaye hata hivyo, hakuwepo.
Alipotafutwa kwa njia ya simu na
kuulizwa kuhusu suala hilo, afisa uhusiano huyo aliyejitaja kwa jina la
Walter Rodney Luanda, alisema kwa sasa yupo mkoani Kilimanjaro kwa
shughuli za kiofisi hivyo suala hilo atalizungumzia akipata nafasi.
Hata
hivyo, OFM ilizungumza na kiongozi mmoja wa wanafunzi aliyeomba hifadhi
ya jina lake na kukiri uwepo wa udhaifu huo lakini alisema usalama
chuoni hapo ni mkubwa kwa vile wanafunzi wamepewa elimu ya ulinzi
miongoni mwao kwa kuripoti jambo lolote wanalotilia shaka.
Note: Only a member of this blog may post a comment.