Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe.
Hans Mloli, Dar es SalaamMWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, ametangaza kujitua zigo la kuisuka timu hiyo, baada ya kukamilika kwa usajili wa wachezaji waliohitajika na sasa kibarua kimewaangukia kamati ya mashindano ya timu hiyo na benchi la ufundi lililo chini ya Muingereza, Dylan Kerr.
Kauli hiyo ya mwenyekiti huyo inakuja baada ya kufanikisha kwa kiasi kikubwa usajili wa wachezaji waliokuwa wakihitajika kikosini hapo kabla dirisha la usajili halijafungwa usiku wa Jumapili ya wiki iliyopita. Lakini dirisha la wachezaji wa kulipwa linatarajiwa kufungwa Septemba 6, mwaka huu.
Akizungumza na Championi Jumatano, Hans Poppe alisema kwa upande wake amemaliza kila kitu alichokuwa anahitajika kukifanya, baada ya kufanikiwa kuinasa saini ya mshambuliaji wao mpya, Msenegali, Pape N’daw na kuachana na Makan Dembele raia wa Mali aliyegoma kufanya majaribio.
“Kwa upande wangu nimeshamaliza kila kitu, ilikuwa ni kumnasa mmoja kati ya N’daw au Dembele na mwisho wake akawa ni N’daw, baada ya hapo kwenye upande wetu tumemaliza majukumu yetu ya kusajili.
“Kilichobaki mambo mengine ni kamati za mashindano na benchi la ufundi katika kujipanga vizuri kwa ajili ya msimu ujao,” alisema Hans Poppe.
Katika dirisha hili kubwa lililofunguliwa tangu Juni 15 na kufungwa Agosti 30, mwaka huu Simba imefanikiwa kuwanasa Peter Mwalyanzi kutoka Mbeya City, Mohammed Fakhi (JKT Ruvu), Musa Mgosi (Mtibwa Sugar), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya ya Qatar), Joseph Kimwaga (Azam) na Haji Nuhu (huru).
Wengine wa kimataifa ni Vincent Agban wa Ivory Coast, Mzimbabwe, Justice Majabvi, Mrundi, Emiry Namubona, Mganda, Hamis Kiiza na N’daw watakaoungana na Waganda, Juuko Murshid na Simon Sserunkuma waliokuwepo tangu msimu uliopita.

Note: Only a member of this blog may post a comment.