Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza na wahariri wa vyombo vya
habari, nyumbani kwake, Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hana mpango wa kuhama Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na iwapo kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, ni
vyema akahama kwa sababu yeye hana mpango huo.
Lowassa alitoa kauli hiyo alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari
nyumbani kwake mjini Dodoma jana ambako alieleza mambo mbalimbali
kuhusu afya yake, suala la Richmond, elimu, ajira, utajiri wake na hali
ya kisiasa kwa ujumla.
Hata hivyo, Mbunge huyo wa Monduli hakutaka kujibu maswali mengi kwa
madai kuwa atazungumza Jumamosi mjini Arusha atakapotangaza nia yake ya
kugombea urais.
Kuhama CCM
Alipoulizwa iwapo yupo tayari kuhama CCM na kwenda upinzani
asipopitishwa na chama hicho kuwania urais alisema: “Sina mpango wa
kuhama chama changu, sina plan B, mimi ni plan A tu, tangu nimemaliza
Chuo Kikuu mwaka 1977 nimekuwa mwana-CCM, sijafanya kazi nje ya CCM
ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo
cha Mikutano cha Arusha (AICC). Maisha yangu yote yapo CCM.
“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi,” alisema.
Kimya miaka saba
Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya
mtambo wa kufua umeme wa Richmond, alisema kimya chake baada ya tukio
hilo kilitokana na siasa nyingi za uhasama na kutishiana.
“Kwa miaka saba, niliona ni hekima kunyamaza, askofu mmoja alinifundisha
kuwa ukimya ni hekima kutoka kwa Mungu. Nilichagua kuwa kimya.
Nilinyamaza kwa sababu ilikuwa salama kunyamaza, ningezungumza ningeweza
kutibua mambo kwenye nchi na kusababisha mambo ambayo hayapo.
“Nilinyamaza ili kuipa muda Serikali ifanye kazi yake…. sikupenda
kuzungumza kwa sababu ya siasa nyingi za uhasama na kutishiana kwingi,
kuna kusingiziana kwingi, kufitiniana kwingi. Kukaa kimya ni jambo gumu
sana kwa mwanasiasa, lakini nashukuru Mungu niliweza hilo,” alisema
Lowassa ambaye Jumamosi atatangaza nia ya kuwania urais mjini Arusha.
Wagombea wapime afya
Wagombea wapime afya
Alipoulizwa kuhusu madai kuwa afya yake inaterereka, alisema anaamini yupo fiti na akashauri wagombea urais wote wakapimwe.
“Hata nikikimbia kilomita 100 watasema mimi mgonjwa. Hivi karibuni
nilitembea kilomita tano na albino jijini Dar es Salaam, kuna watu
wakasema nimechoka sana, nimepata ‘stroke’ na nimekimbizwa Ujerumani
kutibiwa, huo ni upuuzi mtupu. Kuna chuki imeingia katika siasa zetu na
kutakiana mabaya. Afya ni neema kutoka kwa Mungu tu. Napenda
kuwahakikishia kuwa nipo fiti na nipo fiti na kwa lolote. Nadhani ni
wakati sasa kwa chama chetu waweke utaratibu wanaogombea nafasi hii
ambayo nitaitangaza Jumamosi, tukapime wote afya na mimi nitakuwa wa
kwanza kujitokeza kwenda kupima.
“Twendeni tukapime tuone nani mgonjwa. Tuonane kwenye uwanja wa
mapambano katika mchakamchaka wa maendeleo, ninajua nitawashinda kwa
mbali,” alisema.
Sakata la Richmond
Kuhusu sakata la Richmond, ambalo lilimfanya ajiuzulu uwaziri mkuu,
Lowassa alisema tatizo kubwa halikuwa kuhusu mitambo hiyo ya umeme ila
uwaziri mkuu.
“Ajenda haikuwa kuhusu Richmond, ila uwaziri mkuu ndiyo maana
niliwaachia. Tunajifunza nini katika hilo, wakubwa wawili wa Marekani,
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje (Hillary) Clinton na Rais wake (Barack)
Obama, wote wamekuja Tanzania na wamethibitisha kuwa ile mitambo ni
mizuri. Lakini jingine tulilojifunza katika ubishi ule umeisababisha
nchi hasara ya Dola 120 milioni,” alisema Lowassa.
“Moja ya ushauri wangu wakati ule ilikuwa ni kutaka kuvunja mkataba wa
Richmond nikaita wataalamu, nikawaelezea kuhusu habari za magazeti kuwa
zinasema hawa jamaa (Richmond) hawana fedha, hebu angalieni, nikaita
wataalamu na mwanasheria mkuu, nikawaambia kuna hii habari kuweni
makini, pamoja na hayo nikaweka kwa maandishi kwa mwanasheria mkuu, pia
kulikuwa na timu ya mashauriano ya Serikali iliyokuwa chini ya makatibu
wakuu nao walikuwa na vikao vyao, ilikuwa inaongozwa na (Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha (Gray Mgonja) nao wakakutana chini ya Katibu Mkuu
Kiongozi na baada ya kukutana wakatoa uamuzi ambao sina haja ya
kuujadili. Lakini ubishi ule umetugharimu Dola 120 milioni.
“Nilipotaka mkataba uvunjwe nilikuwa nimetoa uzoefu wangu kwani kabla ya
kuwa waziri mkuu nilikuwa nimekuwa waziri wa maji na mifugo ambako
nilivunja mkataba wa kampuni ya Kiingereza iliyokuwa imewekeza katika
mradi wa maji Dar es Salaam ya City Water.
“Chini ya uongozi wa Rais (Benjamin) Mkapa tukagundua hawa jamaa (City
Water) ni matapeli…tulifanya kikao saa tisa alasiri, tukachukua kibali
cha kumkamata yule Mzungu wa City Water na tukamfukuza akaondoka siku
hiyohiyo kwa ndege kurudi kwao, tulifanya saa tisa alasiri ili asiende
mahakamani kupata zuio, kwa hiyo tulivizia muda huo ili asije kwenda
kupata zuio.
Nini tofauti ya Lowassa nje ya Serikali na ambaye angeendelea kuwa
waziri mkuu na kisha kugombea urais? “…Naamini kuwa kama tungeanza kwa
kasi ile tuliyoanza nayo nikiwa waziri mkuu, sasa ningepita napunga
mkono ningepata kura zote… lakini kinachonisikitisha tumekuwa hatufanyi
maamuzi magumu au rahisi, kila kitu kinakwenda legelege. Rais amefanya
jitihada kubwa, lakini kuna mambo katika nchi hayaendi, matokeo yake
Uganda, Kenya na Rwanda zinatupita sasa, haifai, lakini nawaachia uhondo
nitaelezea vizuri Jumamosi, Arusha.”

Note: Only a member of this blog may post a comment.