Kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto.
Omary Mdose, Dar es Salaam KOCHA
Mkuu wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, amefunguka kuwa kikosi chake
sasa kimeiva na kipo tayari kwa mapambano huku akidai kuwa wachezaji
wake wote wapo kwenye kiwango cha juu.Kerr ameyasema hayo huku kikosi chake kikiwa tayari kimeshacheza mechi tatu za kirafiki huko visiwani Zanzibar na kufanikiwa kushinda zote, keshokutwa Jumatano kikosi hicho kinatarajia kupambana na KMKM katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
“Rafiki yangu napenda kukwambia kwa sasa sina partnership ambayo ni hatari kuzidi nyingine, bali kila mchezaji nikimpanga na mwenzake wanacheza vizuri tu na hiyo ndiyo nilikuwa nahitaji iwe hivyo,” alisema Kerr.
Lakini kocha wa viungo wa Simba, Mserbia, Dusan Momcilovic, amesema: “Huyu (Mwinyi) Kazimoto ni hatari sana.” Baadaye kocha huyo akatamka kuwa anampa miezi miwili tu na baada ya hapo kiungo huyo atakuwa fiti kabisa na moto wa kuotea mbali.
Kazimoto aliyewahi kuichezea Simba miaka ya nyuma kabla ya kutimkia Qatar na kuitumikia Klabu ya Al Markhiya ya nchini humo, alirejea nchini mwishoni mwa mwezi uliopita na kujiunga tena na Simba huku akipewa mkataba wa miaka miwili.
Ili kumrudisha kwenye kiwango chake, kocha huyo amempa muda wa takriban miezi miwili tangu alipojiunga na Simba ambapo baada ya hapo anaamini atakuja kuwa msaada mkubwa kikosini hapo na mwisho wa siku kuipa mataji mbalimbali.
“Kwa sasa uwezo wake ni asilimia 70. Kutokana na kuwa, hivyo hata akicheza mechi basi atatumia dakika 50 mpaka 60 kucheza kwa kiwango kizuri, lakini atakapokuwa sawa basi atakuja kuwa mmoja kati ya wachezaji tegemeo kikosini,” alisema Momcilovic.
Mzimbabwe mpya wa Simba...
Licha ya kiungo mpya aliyejiunga na Simba kwa ajili ya majaribio, Mzimbabwe, Justice Majabvi, kutoanza mazoezi na wachezaji wa Simba huko visiwani Zanzibar, lakini kocha mkuu wa kikosi hicho, Muingereza, Dylan Kerr, amemtaja kiungo huyo kuwa ni mtu sahihi.
Majabvi aliwasili nchini juzi Jumamosi na kujiunga moja kwa moja na kambi ya Simba iliyopo Zanzibar ambapo amepewa muda wa kufanya mazoezi na kikosi hicho na kama akiliridhisha benchi la ufundi la timu hiyo, atapewa mkataba na kuimarisha safu ya kiungo.
“Ni mchezaji mzuri wa kimataifa na kama akifanikiwa kujiunga nasi, basi naamini ataisaidia timu kufanya kile ambacho tunakitarajia wote ikiwemo kwenye harakati za kusaka mataji msimu ujao,” alisema Kerr.
Naye kocha wa viungo wa timu hiyo ambaye kitaaluma ni profesa wa masuala ya viungo vya wachezaji, Mserbia, Dusan Momcilovic ‘Dule’, amemzungumzia mchezaji huyo kwa kusema kutokana na jinsi alivyomuona licha ya kutofanya mazoezi, anaamini yupo fiti lakini atampa kwanza mtihani mdogo kabla ya kutoa jibu kamili juu ya uwezo wake.

Note: Only a member of this blog may post a comment.