Friday, August 14, 2015

Anonymous

NI HATARI SANA! Dawa Zanaswa Zikiuzwa Kiholela Jijini Dar

OFM DAWA (2)
Ramadhani na Mayasa Mariwata
NI hatari! Shirika la Afya la Dunia (WHO) limetoa ripoti  na kubainisha kwamba  dawa za kutibu maradhi ya kuharisha, vichomi, maambukizi ya kwenye njia ya mkojo (U.T.I), mafua na magonjwa kama ya zinaa mfano kaswende na kisonono sasa zimekuwa sugu.
Taarifa hiyo imesema kuwa, bakteria wanaoeneza maradhi hayo kwa sasa wanaua binadamu wengi kuliko ugonjwa wa Ukimwi ambao hadi sasa hauna tiba wala chanjo.
OFM DAWA (4) 
Lakini kuna taarifa kuwa, matumizi mabaya ikiwemo wafamasia kwenye maduka ya dawa baridi na famasi mbalimbali kuuza madawa hayo kwa wateja (wagonjwa) bila kupata maelekezo au vyeti kutoka kwa madaktari ambako wagonjwa hao wametoka, yamechangia vifo au madhara makubwa kwa watumiaji.
Kumekuwa na madai mbalimbali kutoka kwa vyanzo vya gazeti hili kuwa, baadhi ya famasi jijini Dar zimekuwa zikiuza dawa kali kama antibiotcs  kwa watu bila kuwa na vyeti vya hospitali.
OFM DAWA (1)Dawa kama Diazepam (Valium), Cipro (Ciprofloxacin), Ampiclox na nyingine nyingi za hivyo, zimekuwa zikiuzwa kwa wateja licha ya kwamba, matumizi yake yanataka maelekezo ya daktari na pia dawa hizo zina madhara kwa upande wa pili (side effects).
Kama ilivyo kawaida ya makamanda wa kikosi maalum cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) wa Global Publishers, Jumatatu iliyopita walitembelea baadhi ya maduka yanayouza dawa baridi na kununua dawa ambazo zinaweza kuua kama zikitumiwa vibaya huku wauzaji wake wakihudumia bila ya kudai cheti kutoka kwa daktari.
OFM DAWA (3)OFM walianza ziara yao saa 8:09 mchana katika maeneo ya Manzese, Dar ambapo makamanda hao walitia timu kwenye duka la kwanza lililopo jirani kabisa na Kituo cha Daladala cha Big Brother na kununua vidonge aina ya Valium ambavyo hutumika kama dawa ya usingizi.
Huku akirekodiwa, muuzaji wa duka hilo aliwauzia makamanda hao dawa hizo bila kuuliza nani anakwenda kutumia na kutotoa maelekezo yoyote kuhusu matumizi yake.
OFM DAWA (5)
Saa 8:18 mchana, makamanda wa OFM waliingia kwenye duka lingine na kufanikiwa kununua dawa aina ya Cipro ambazo hutumika kutibu magonjwa mbalimbali kama maambukizi ya mfumo wa mkojo (U.T.I), homa ya matumbo (Typhoid), kichomi na maambukizi ya ngozi na mengine mengi.

Huko nako makamanda wetu waliuziwa dawa hizo bila ya kupata maelekezo yoyote mpaka pale kamanda mmoja alipoanza kuuliza matumizi sahihi ya dawa hizo ambapo alisema yeye aliagizwa na ndugu yake ambapo muuzaji alifafanua kidogo kuwa ni dawa inayotumika kutibu maambukizi ya mfumo wa mkojo na kuongeza kuwa, huleta athari kwa mama mjamzito ambayo inaweza kusababisha mimba kuchoropoka.

“Hii dawa ni hatari, yaani ni kali sana mtu akitumia hivihivi asipoangalia inaweza kumpeleka (kufa) maana inalegeza sana. Inabidi achanganye na dawa inayoitwa Azuma inapoza makali, kama mtu ana ujauzito haifai kunywa Cipro maana akinywa mimba inaweza kutoka,”alisema dada huyo.

Makamanda wetu waliendelea na kazi ambapo waliingia duka jingine lililopo maeneo hayo na kununua dawa aina ya Ampiclox ambayo hutumika kutibu kifua, typhoid na magonjwa mengine yanayoenezwa na bakteria.
Muuzaji wake alionekana kujikanyaga katika maelekezo ya matumizi kwa kumpigia simu mtu aliye mbali na duka hilo ili ampe maelekezo.

Baadaye, OFM lilizungumza na Dokta Chale wa hospitali moja ya jijini Dar ambapo alisema: “Kwa kawaida, dawa yoyote ambayo ni antibiotic haitakiwi kuuzuwa famasi bila maelekezo kutoka kwa daktari. Kwani dawa nyingi ni hatari.

Pia dawa hizo ni sumu. Lazima daktari ajue mwili wako kama unatakiwa kumeza dawa hizo. “Unajua maduka ya dawa siku hzi wanakosea sana. Siku hizi mtu anakwenda famasi, anataja dawa hizo, anauziwa. Si sawasawa. Bodi ya Chakula na Madawa (TFDA) lazima iangalie hili,” alisema daktari huyo. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seleman Seif Rashid alipopigiwa simu juzi ili azungumzie hilo, hakuwa hewani.
Juhudi za kumtafuta waziri huyo bado zinaendelea.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.