Donald Ngoma
Derick Lwasye,MbeyaYANGA ipo jijini Mbeya ikijiandaa na msimu mpya wa 2015/2016 lakini habari nzuri kwa Wanayanga ni kuwa staika wao mpya, Donald Ngoma anaonekana kuwa na nyota njema klabuni hapo kutokana na mashabiki kumkubali.
Ngoma ambaye bado hajawa na kasi ya kutisha katika kufunga, tayari ameshaonyesha dalili nzuri kutokana na kuonyesha uwezo mzuri katika mechi mbili za kirafiki jijini hapa ambazo ni dhidi ya Kimondo FC na Tanzania Prisons ambazo zote Yanga ilishinda.
Katika mechi ya juzi dhidi ya Prisons, mashabiki wengi wa Yanga na hata wale ambao hawakuwa wa timu hiyo, walionekana kuvutiwa na kiwango kilichoonyeshwa na Ngoma ambaye ni raia wa Zimbabwe.
Ngoma alionekana kuwa mwiba mkali kwa walinzi wa Prisons kiasi cha kuwa msumbufu mara kwa mara ambapo alikuwa akishirikiana vema na straika mwenzake wa kati, Amissi Tambwe, hali iliyoonyesha kuwa kocha wao, Hans van Der Pluijm anaweza kuutumia ushirikiano wao kama pacha katika msimu ujao.
Wakizungumza mara baada ya mechi hiyo ya juzi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine na Yanga kupata ushindi wa mabao 2-0, mashabiki hao waliokuwa na furaha ya ushindi, walisema hakuna timu ya kuwazuia katika harakati za kuchukua ubingwa msimu ujao.
“Msimu huu ni wetu, hakuna timu itakayoweza kuzuia mziki wetu, si umemuona Ngoma alivyokuwa akiwasumbua mabeki? Hata kama hakufunga lakini bado ameonyesha kuwa anao uwezo mkubwa wa kutufikisha mbali, watani zetu wakae mkao wa kupokea dozi tu safari hii,” alisema shabiki mmoja huku akiungwa mkono na wenzake.
Baada ya ushindi dhidi ya Prisons, Yanga itarejea uwanjani hapo, keshokutwa Jumapili kukipiga na Mbeya City ambao nao ni wapinzani wao wa ligi kuu kama ilivyo kwa Prisons.
Note: Only a member of this blog may post a comment.