Kadhalika Takukuru inashikilia kiasi cha Sh. 1,677,000 kilichokutwa kwa makada hao kupitia mtego uliowekwa kwenye majimbo ya Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Makada hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) kata ya Goba, Pili Mustafa, aliyekamatwa saa 3 usiku akiwa na Sh. 1,330,000, Rehema Luwanja, anayegombea udiwani kata ya Goba na Sh. 95,000, huku akiwa ameshagawa 110,000.
Wengine ni Katibu Itikadi wa CCM kata ya Kibamba, Babu Kimanyo, aliyekamatwa saa 4:30 usiku akiwa na Sh. 252,000 na tayari alishagawa sh. 330,000, Katibu CCM kata ya Kibamba, Elias Nawera ambaye anagombea Ubunge Kawe, Siraju Mwasha anayegombea udiwani Msigani.
Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, Denis Manumbu, alisema kuwa mbali na watuhumiwa hao, wamepokea malalamiko 28 yanayohusu rushwa ambayo wanayafanyia uchunguzi ili hatua zichukuliwe.
Alisema katika kipindi hiki cha kura za maoni za kuwapata wagombea katika ngazi ya udiwani na ubunge katika vyama vya siasa majimbo manne ya Wilaya ya Kinondoni, ofisi yake imepokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi zinazohusu vitendo vya rushwa.
Manumbu alisema vitendo hivyo vinafanywa na watangaza nia na wapambe wao na baada ya kupitia taarifa hizo ofisi ilizifanyia kazi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao na kuwahoji.
Alisema ofisi yake ina mamlaka kisheria ya kumuita mtu yeyote kutoa maelezo ili kusaidia uchunguzi wa tuhuma husika na mamlaka hayo kwa mujibu wa kifungu cha 10(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, atakayekiuka wito huo atakuwa amekwenda kinyume cha sheria.
Hata hivyo, alisema Takukuru inafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria na hawatasita kumchukulia hatua mgombea wa chama chochote na upelelezi utakapokamilika watafikishwa kwenye vyombo vya dola.


Note: Only a member of this blog may post a comment.