Tuesday, August 18, 2015

Anonymous

INATISHA SANA! Mke Apasuliwa Kichwa na Mumewe, Afariki Dunia!

Na Gregory Nyankaira, Mara
MWANAMKE mmoja aliyejulikana kwa jina la Pendo Idd Mande (37), mkazi wa Kitongoji cha Nyamika, Kijiji cha Mwikoro, Kata ya Buruma wilayani Butiama, Mara ameuawa kikatili kwa kupasuliwa kichwa kwa panga na mumewe aitwaye Amos Kiginga (pichani) kwa kile kilichodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Tukio hilo la kinyama lilijiri Agosti 13, mwaka huu, saa 4:30 usiku kwenye sherehe ya kujenga makaburi.
Kwa mujibu wa mashuhuda, kabla ya kukutwa na mauti, Pendo aliondoka nyumbani kwa wazazi wake, saa 2 asubuhi kwenda kwenye sherehe hiyo iliyofanyika kwa jirani yao ambako alikaa hadi usiku.

Mashuhuda hao walisema kuwa, ilipofika saa 4 usiku, Amos alimfuata Pendo kwenye sherehe hiyo na kumtaka warudi nyumbani kulala, lakini mwanamke huyo aligoma kwa madai kuwa, alipewa jukumu la kukusanya vyombo vilivyotumika na kuviosha.

“Baada ya Amos kutumia kila njia aondoke na Pendo lakini ikashindikana, ndipo alipochomoa panga kwenye koti lake na kumkata nalo kichwani mke wake huyo na kukipasua kisha akatokomea kusikojulikana na kumwacha Pendo akigaragara chini na hatimaye kupoteza uhai huku wananchi waliokuwa kwenye sherehe hiyo wakiduwaa bila kutoa msaada wowote,” kilisema chanzo kimoja.

Baba mzazi wa marehemu Pendo, Idd Mande (62) alipozungumza na gazeti hili alisema, Amos alikuwa akiishi na binti yake bila kufunga naye ndoa japokuwa kiserikali ni mkewe kwa kuwa waliishi miaka mingi.

Alisema alijua kuwa, kijana huyo alikuwa akiishi na binti yake kwa kipindi kirefu na kuzaa naye watoto wawili na alikuwa akiingia nyumbani hapo bila kikwazo chochote na kupewa heshima ya mkwe lakini anashangaa siku hiyo ya tukio Amos kubadilika kiasi hicho mpaka kumuua mwanaye kwa sababu ya wivu.

“Yeye alijua binti yangu alipogoma kuondoka alikuwa amepata hawara pale kwenye shughuli. Tayari nimefungua kesi ya mauaji katika Kituo cha Polisi cha Butiama na kupewa jalada kumbukumbu namba BUT/RB/908/2015 KUUA. Namtafuta huyu muuaji hadi nimpate ili nimfikishe kwenye vyombo vya sheria,” alisema Mande.

Polisi wilayani Butiama wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kulifuatilia ili kumkamata mtuhumiwa huyo.
Marehemu Pendo alizikwa Agosti 14, mwaka huu kwenye makaburi ya nyumbani kwao. Ameacha watoto wawili.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.