Makongoro Oging’ na Richard Bukos, Mkuranga
MAPYA tena!
Aliyekuwa askari magereza wa Gereza la Dondwe, Wilaya ya Mkuranga,
Pwani, Juma Rashid ambaye Uwazi liliwahi kumripoti kuwa, ndiye ayechora
ramani yote ya uvamizi na mauaji ya askari wa Kituo cha Polisi
Stakishari, Dar imebainika kwamba ameuawa, Uwazi linazidi kukokotoa.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjJtWdNc6xxDgSTTlKt2J_wsX77W2wh6U6uF1VhxW1UmHkxWylIQ-tMQBqanZHxpLfSpXd_tBuRgkBBF8rxOGlO6xWuUXk-XU_18nG9YABGHC6sEhskm3hc_BstHUxpbBFjSjIk_O9uzBPc/s640/IMG_0387.jpeg)
Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti
hili umebaini kwamba askari huyo ndiye yule aliyeuawa siku ya tukio
lililojiri Julai 12, mwaka huu nje ya kituo cha Stakishari ambaye
alijulikana kwa jina maarufu la Osama.
HAIKUJULIKANA
Hata hivyo, baada ya muaji hayo, taarifa
zilienea kwamba, aliyeuawa eneo la tukio ni mmoja wa majambazi hao bila
kujulikana kuwa ndiye askari magereza mstaafu mpaka hivi karibuni
ambapo, mke wake, Fatuma Hassan (37) alipoanika ukweli kwa gazeti hili.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, siku
chache kabla ya tukio la uvamizi huo, marehemu Osama alionekana kwenye
baa moja iliyopo maeneo ya Stakishari na kuwanunulia pombe baadhi ya
polisi huku akichunguza sehemu zinazohifadhiwa silaha na jinsi gani
polisi wanavyokaa katika lindo pia ni siku gani inafaa kwa uvamizi
ambapo alibaini ni Jumapili.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, timu ya Uwazi
ilifunga safari hadi kwenye Kijiji cha Dondwe na kufikia nyumbani kwa
marehemu Osama ambaye aliacha kazi akiwa na cheo cha koplo na kufanya
mahojiano na mke wake, Fatuma.
Mwanamke huyo ambaye alianza kwa kukiri
kwamba marehemu Osama alikuwa mumewe, alisimulia maisha yake na mwanaume
huyo hadi anauawa. Alikuwa na haya:
“Tulifunga ndoa na Juma mwaka 1999 huko
Kigoma alikokuwa akifanyia kazi katika Gereza la Kwitanga. Tulipendana
sana. Mume wangu alikuwa mpole, msikivu, sikutegemea kama angeweza
kuuawa katika mazingira kama haya ya aibu.
“Mwaka 2009, akatakiwa kuja kuripoti
Gereza la Ukonga (Dar) halafu akapangiwa kuja hapa Gereza la Dondwe (ni
tawi la Gereza la Ukonga).”
AANZA KUBADILIKA TABIA
“Akiwa hapa Dondwe, ghafla mume wangu
alianza kubadilika tabia, akawa anafuga ndevu tofauti na taratibu za
kazini kwake. Akaonywa na viongozi wake lakini hakubadilika.
“Lakini pia alinitaka mimi nianze kuvaa nguo za kufunika mwili mzima mpaka mikono na kubaki uso tu. Hilo sikukubaliana nalo.
“Tuliendelea kuishi mpaka mwaka 2012,
akasema anataka kuacha kazi. Mimi sikukubaliana naye kwa sababu tuna
watoto, yeye akasema lazima aache kazi. Nilimuuliza anataka kufanya kazi
gani na kwa nini aliamua kuacha kazi? Akasema aliamua hivyo kwa sababu
imani ya dini yake haikuwa ikimruhusu kufanya kazi ya uaskari ambayo
aliitafsiri kuwa ni ya ukafiri.
“Kweli. Siku ilifika, akaandika barua ya
kuacha kazi, lakini pia akaniandikia mimi talaka moja kwa sababu
sikumuunga mkono kwenye matakwa yake.”
“Maisha yalianza kuwa magumu. Akawa
anauza maji mitaani kwa kubeba madumu kwenye baiskeli. Baadaye akanunua
pikipiki ya magurudumu matatu, akaendelea na biashara hiyo.”
MKE ARUDI KWAO
“Ilinibidi mimi niondoke kurudi kwetu
Singida. Baadaye nilikwenda kwao kuwaeleza ndugu zake akiwemo baba yake
mzazi. Walishangaa sana, aliitwa lakini hakwenda. Wakanishauri nirudi
hapa Dondwe ili niwatunze watoto. Majirani zangu hapa nao walinipigia
simu wakisema nirudi, watoto wanateseka.
“Nilirudi, lakini nilipofika ikawa kila mmoja analala katika chumba chake. Hakunijali kwa chakula wala kwa mavazi.
“Kitu kilichonishangaza ni kwamba,
aliniambia kuwa anataka kuwatoa watoto kwenye shule za serikali na
kuwapeleka za dini. Nilikwenda kwa mtendaji wa kijiji nikamweleza.
Aliitwa ofisini lakini hakwenda. Kuanzia hapo akaacha kuwahudumia.”
MAAJABU ZAIDI
“Mimi nilianza kuamini mume wangu hakuwa
yule baada ya watu aliokuwa akiswali nao, walipokuwa wakija hapa
nyumbani aliwaambia mimi si mke wake. Isitoshe hata baba yake mzazi
alipofariki dunia Aprili mwaka huu hakwenda.”
STAKISHARI
“Nakumbuka siku hiyo ya tukio la kule
Stakishari, aliondoka hapa jioni akisema anasafiri kwenda kwao Singida.
Nilimuuliza mbona unaondoka na pikipiki, utaitunza wapi? Akasema
ataiacha kwa ndugu zake wa Dar.
“Hata hivyo, nilipata wasiwasi. Lakini
sikuwa na la kusema. Aliondoka zake. Ilipofika usiku nilimpigia simu
ikawa haipatikani. Kwa kweli sikupata usingizi. Kesho yake nikapiga tena
simu pia hakupatikana.
“Niliamua kuwapigia simu kwao, wakasema
hawana taarifa ya ujio wake. Jioni nikampigia dada yake ambaye yupo
Singida mjini, akasema hawajamuona.
MAMBO HADHARANI
“Nilikuwa najiuliza maswali mengi sana
lakini bila majibu. Baada ya siku kama tatu kupita, ikatangazwa na jeshi
la polisi kwamba kuna jambazi mwenye madevu ameuawa na picha yake ikawa
mtandaoni. Mtendaji wa kijiji chetu, Said Mohamed Mfume naye akawa
amepata taarifa hizo akaniita ofisini kwake.
“Mtendaji akaniambia kwamba kuna picha
ya mtu aliyeuawa katika tukio la Stakishari anafanana na mume wangu
lakini hakunionesha. Picha hiyo ilisambaa hadi kwao Singida.
“Kuna ndugu yangu akaja mpaka hapa
Dondwe akanionesha hiyo picha, nikagundua ni yeye mume wangu. Katika
magazeti waliandika jina la Ustadhi Rashid.
“Marafiki zake nao baada ya kupata
taarifa walikuja hapa na kuniambia eti mume wangu ameuawa lakini ni kama
amepata shahada. Wakimaanisha kwamba amekufa kishujaa katika kutetea
dini.”
MKE AENDA STAKISHARI
“Ilitulazimu kwenda Kituo cha Polisi
Stakishari ili kupata taarifa kamili. Kufika wakaniweka ndani siku tano
kwa mahojiano. Hivi ninavyozungumza na wewe simu yangu bado iko pale
kituoni.
“Niliporudi hapa nyumbani, niliwaambia
watoto juu ya kifo cha baba yao, kwa kweli walijisikia vibaya sana
ingawa alikuwa hawataki waziwazi.”
MWILI WACHUKULIWA
“Agosti 4, mwaka huu, mimi na watu
wengine hapa tulikwenda kuuchukua mwili Muhimbili. Kufika tukapata
taarifa kwamba kuna watu walikwenda jana yake kuutaka mwili lakini
walizuiwa. Mimi nilijua ni wale marafiki zake.
“Baada ya kuuchukua mwili tulishindwa
mahali pa kwenda kuuzika kutokana na tukio alilolifanya. Ilibidi
tukamzike kwenye Makaburi ya Kijiji cha Mazinda, Mbuyuni, Chanika ambako
kuna dada yangu kaolewa huko. Mumewe alisema kumzikia Dondwe haitatoa
picha nzuri kutokana na aina ya kifo.
“Agosti 8, mwaka huu, tulikwenda
kujengea kaburi lake, tukakuta kifuu cha nazi kilichoandikwa maneno ya
Kiarabu. Ilinishangaza sana mimi. Hivyo ndivyo ilivyokuwa au ninavyomjua
marehemu Rashid Juma baba wa watoto wangu wanne.”
Baadhi ya askari magereza wa Gereza la Dondwe ambao walikuwa wakifanya kazi na marehemu walipohojiwa na Uwazi walisema wanamtambua marehemu ambapo kazini alikuwa akitumia jina la Antony Gembo.
La Juma Rashid lilikuwa la dini lakini
aliamua kuacha kazi kwani alibadilika akawa tofauti na taratibu za
kijeshi. Alipoambiwa ajirekebishe aliamua kuacha kazi lakini cha
kushangaza hakuchunguzwa anakwenda kufanya kazi gani na kwa nini alikuwa
na kiburi hicho cha kuacha kazi.
Baadhi ya wanakijiji waliohojiwa
kuhusiana na maisha ya marehemu huyo walisema hakuna aliyejua angeweza
kujiunga na tabia hiyo ya kihalifu na hata siku alipouawa haikujulikana
mara moja kuwa ni yeye.
Vyanzo vyetu vilieleza kwamba, marehemu
kabla hajabadilika tabia alikuwa akiswali katika nyumba moja ya ibada.
Baada ya muda kukatokea kundi la watu ambao ni marafiki zake kutoka
kijiji jirani.
Hata hivyo, waumini wa madhehebu
waliyokuwa wakiswali waliwashtukia kutokana na elimu ya dini waliyokuwa
wakiitoa ambayo ilikuwa ya kihalifu zaidi, wakatimuliwa.
Inadaiwa kuwa, baada ya kutimuliwa, watu
hao wakiwa na marehemu walielekea Kijiji cha Mandikongo ambapo kulikuwa
na ngome yao. Na ndiko ambako baada ya uvamizi wa Stakishari, jeshi la
polisi lilikuta bunduki 15 na shilingi zaidi ya milioni mia moja na
sabini elfu zikiwa zimefukiwa ardhini.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar,
Suleimani Kova (pichani), aliliambia gazeti hili kwamba baadhi ya
watuhumiwa wa tukio hilo wameshakamatwa.
MTENDAJI WA KIJIJI
Mtendaji wa Kijiji cha Dondwe, Mfume
alipohojiwa na waandishi wetu alikiri kumtambua marehemu kwani alikuwa
mkazi wake na mke wake walikuwa wakifika ofisini kuelezea mambo
aliyokuwa akifanyiwa na marehemu.
Note: Only a member of this blog may post a comment.