NI kweli hujafa
hujaumbika! Leo unaweza kuamka mzima lakini kesho ukafika ukiwa huwezi!
Unaweza kusema ‘mi naumwa’ kumbe hujawaona wagonjwa wenyewe.
Ukishawaona, utagundua kuwa, ugonjwa wako hahuitaji tabibu.
Akizungumza kwa uchungu wa mateso ya
mwanaye, baba mzazi wa kijana huyo, mzee Revocatus Machanga alisema kuwa
maisha ya nyumbani hapo yamekuwa ya huzuni kwani kila anapomuangalia
mtoto wake huyo, machozi yanamtoka.
Mzee Machanga alisema kuwa, mtoto wake
huyo alianza kuugua Novemba 2014. Anasema kijana huyo alianza kwa
kulalamikia maumivu ya kichwa kwamba kinamgonga sana. Pia macho yalianza
kuvimba kidogokidogo, yeye akajua ni ugonjwa wa macho tu na yatapona.
HALI MBAYA, AMPELEKA HOSPITALI
Mzazi huyo aliendelea kusema kuwa, siku
zilivyozidi kwenda mbele, ndivyo macho hayo yalivyokuwa yakizidi
kuvimba. Ndipo aliamua kumpeleka Hospitali ya Macho ya Comprehensive
Community Based Rehabilitation in Tanzania (CCBRT) ambapo waligundua
kuwa macho hayana tatizo ila mishipa ya fahamu ndiyo ina kasoro, hivyo
walishauri apelekwe Hospitali ya Taifa Muhimbili Taasisi ya Magonjwa ya
Mifupa ‘Moi’ (Muhimbili Orthopeadic Institute) ambako kuna wataalam wa
mishipa ya fahamu.
MAJIBU YA MOI
“Tulipofika Moi walimwangalia,
wakampangia siku ya kumuona ambapo ilikuwa kama mwezi mmoja mbele.
Lakini tulipokuwa tukisubiri muda wa kumuona, macho yalizidi kuwa katika
hali mbaya ambapo yalitoka nje kabisa.
ATAKIWA KUPASULIWA
(huku akifuta machozi) mzazi huyo
aliendelea kusema: “Siku ya kumwona daktari ilifika, tukaenda. Walimpima
na kugundua kuwa, ana uvimbe kwenye ubongo wa mbele. Wakasema wanaweza
kumfanyia upasuaji lakini masharti waliyotueleza kuhusiana na upasuaji
huo ni magumu sana.
“Walisema kuwa akifanyiwa upasuaji huo
lazima awekwe chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa muda wa siku kumi
na nne na kwamba atatolewa macho yote na sura yake itabadilika kitu
ambacho kilinifanya nijishauri tena.”
Mzazi huyo ambaye muda mwingi kwake ni
kilio, aliendelea kusema kuwa awali walijua tatizo kubwa ni kansa lakini
kumbe haikuwa hivyo na kwa sasa, uvimbe huo umesababisha pua za kijana
huyo kuziba na meno kuuma kiasi ambacho anashindwa kula chakula zaidi ya
uji na mtori tu.
BABA AULIZIA MATIBABU INDIA
Mzee Machanga alisema kuwa, ilibidi
aulizie hospitali za India zinawezaje kufanya upasuaji huo ambapo wenye
uzoefu walisema kijana huyo anaweza kufanyiwa upasuaji kwa shilingi
milioni 40 kitu ambacho wao kama familia hawawezi kwa kuwa mzazi huyo na
yeye ni mgonjwa, hafanyi kazi yoyote.
MGONJWA AZUNGUMZA KWA TABU
Akizungumza kwa tabu sana na gazeti
hili, Abel alisema anatamani kuwa mzima kama zamani ili aweze kutimiza
ndoto zake kwa kusoma sana. Alikuwa akisomea masoko kwenye Chuo cha
Elimu ya Biashara (CBE) cha jijini Dar.
“Hii hali mimi inaniuma sana. Kuna
wakati najiuliza sasa kwa nini naishi kama kuishi kwenye ni kuteseka
kiasi hiki. Kwa nini mimi? Ingawa najua Mungu ana mipango yake na
ananiona ninavyoteseka.
“Ndoto zangu zote zimekatika kabla ya
kufika mwisho. Ni kama mtu anayeota ndoto akiwa amelala halafu akaamshwa
ghafla. Nilikuwa nikisoma pale CBE ili na mimi niwe na maisha mazuri,
niwasaidie wazazi wangu. Kwa sasa ndoto zangu zimeishia hapa. Lakini kwa
jinsi baba alivyonihangaikia ili nipone, naamini kwa sasa wa kuniokoa
ni Mungu tu,” alisema Abel.
KAMA UMEGUSWA
Ndugu msomaji, kama umeguswa na
tatizo la kijana Abel, unaweza kumsaidia. Baba yake ameeleza kila kitu.
Kinachotakiwa ni pesa tu. Na Kutoa ni moyo si utajiri. Kama unatoa,
unaweza kutumia namba za simu za baba yake ambazo ni; 0713 275740, 0784
275740, 0752 275740.
Note: Only a member of this blog may post a comment.