Deogratius Mongela na Chande Abdallah
MAPENZI yana-run dunia! KATIKA
hali ya kushangaza, Imam wa msikiti mmoja uliopo Kibamba, nje kidogo ya
Jiji la Dar es Salaam aliyefahamika kwa jina moja la Ustadh Anuary, yupo
hoi kwa kuhitaji penzi la muigizaji nyota, Wastara Juma, Risasi
Mchanganyiko linakujuza.
Kwa mujibu wa chanzo chetu makini, Ustaadh Anuary, mwenye elimu ya kutosha ya Dini ya Kiislamu, aliyoipata Dubai, Oman na Zanzibar, amekuwa akimpenda sana muigizaji huyo tangu mwaka 2005, ambaye wakati huo, alikuwa akiishi na mumewe, Juma Kilowoko aliyefariki dunia mwaka 2012.
“Kuna kipindi huwa anachanganyikiwa kabisa kiasi cha hata kumtaja binti huyo wakati wa swala, kiasi cha kuwashangaza waumini. Tunawaombeni mje kumsaidia maana hali yake inazidi kuwa mbaya, inaonekana kama vile ameathirika kisaikolojia,” kilisema chanzo chetu, kinachoswali msikiti mmoja na ustaadh huyo.
Gazeti hili lilimtafuta Ustaadh Anuary na kufanikiwa kumkuta katika moja ya misikiti anayoswalisha na kukiri kuwa ni kweli anampenda Wastara na kwamba alianza kumuweka moyoni mwake tangu mwaka 2005.
“Baada ya kufariki mumewe hali yangu ilibadilika kabisa kiasi cha kuniharibu ubongo wangu, kuna wakati niliharibu hata swala zangu na kushindwa kuendelea na mafundisho ya dini. Najaribu kuangalia filamu zake, muda mwingine nanunua hata magazati yenu ilimradi nione sura yake,” alisema mwanaume huyo na kuongeza kuwa angependa kumuoa.
Alisema hata kama binti huyo aliyemsifu kwa mavazi yake ya heshima anamzidi kipato, bado anaamini atamfaa kwani atafuata dini kutokana na kujiheshimu kwake.
Alizidi kumwaga ubuyu kuwa katika kumpenda kwake kusiko kawaida, kuna wakati alilazimika kwenda Hospitali ya Tumbi Kibaha, ambako daktari mmoja, alimweleza ili hali yake ya kawaida irejee ni lazima akutane na mrembo huyo.
Gazeti hili lilijaribu kuwasiliana na muigizaji huyo ambaye ameukosa ubunge wa Viti Maalum kupitia CCM hivi karibuni, lakini hadi tunakwenda mtamboni hakuweza kupatikana licha ya simu yake kuita kwa muda wote.

Note: Only a member of this blog may post a comment.