Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya
Simanjiro mkoani Manyara imezidi kupata pigo baada ya Mahakama kutengua
matokeo ya uchaguzi wa wenyeviti wa vitongoji 16 vya mji mdogo wa
Mirerani, kwa maelezo kuwa ulikiuka sheria na utaratibu wa Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha
mwezi mmoja kwa Mahakama kutengua matokeo ya uchaguzi huo ambao
uliwaweka madarakani makada wa CCM.
Awali, Mei 30 Mahakama ya Hakimu Mkazi
Wilaya ya Kiteto ilitengua matokeo ya uchaguzi wa mwenyekiti wa Kijiji
cha Lobosireti kwa kukiuka sheria na utaratibu.
Chadema ilifungua kesi kadhaa mahakamani
hapo kupinga kitendo cha wagombea wa CCM kupewa ushindi bila kufanya
uchaguzi Desemba 14, mwaka jana.
Hukumu hiyo ya jana, inatokana na kesi
zilizofunguliwa na Chadema wilayani Simanjiro kwenye kata za Endiamtu na
Mirerani, wakipinga wagombea wa CCM kupewa ushindi bila kupigiwa kura
kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana.
Hakimu Mkazi Mfawidhi mahakama hiyo, Elimo Massawe
aliagiza kurudiwa kwa uchaguzi wa viongozi wa vitongoji vya Zaire,
Kisimani, Tenki la Maji, Endiamtu, Kairo na Kazamoyo vilivyoko Kata ya
Ediamtu.
Hakimu Massawe alitaja vitongoji vingine
kuwa ni Sekondari, Kilimahewa, Tanesco, Kazamoyo Juu, Mji mpya,
Tupendane na vitongoji vya Kata ya Mirerani ambavyo ni Kangaroo,
Songambele A, Getini na Songambele B.
Katika kesi hiyo, Chadema iliwakilishwa na mawakili James Millya, Shadrack Kimomogoro na Daudi Haraka na Mahakama iliamuru walipwe Sh160 milioni za gharama za kesi hiyo ambayo ilichukua takribani miezi sita hadi kutolewa hukumu.
Katibu Mwenezi wa Chadema mkoani Manyara, Ambrose Ndege
alisema Mahakama imetenda haki kwa kutoa hukumu sahihi na wanajipanga
ipasavyo kuhakikisha watashinda vitongoji vyote pindi uchaguzi huo
utakaporudiwa.
“Tuliwaeleza
tangu awali kuwa uchaguzi ukifanyika tutawashinda saa nne asubuhi hivyo
tunawasubiri uwanjani na tutaongoza Mamlaka ya Mji wa Mirerani kwani
wananchi wanatukubali,” Ndege.
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa CCM wa Kata ya Endiamtu, Mashaka Jeroro
alisema wanatarajia kukata rufaa kupinga hukumu hiyo akisema wagombea
wa Chadema walikosea kujaza fomu ndiyo sababu wakawekewa pingamizi.


Note: Only a member of this blog may post a comment.