Mwalimi wa Shule ya Msingi Kibumaye iliyopo tarafa ya Inchage wilayani Tarime mkoani Mara, Nelson Zachma amekufa kwa kujitosa Ziwa Victoria.
Ilidaiwa kuwa mwalimu huyo alifanya
uamuzi huo wa kujitosa majini alipokuwa safarini akitokea eneo la Kinesi
kwenda Musoma mjini kwa kutumia usafiri wa kivuko.
Kaimu Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Sweetbert Njewike
alisema kuwa tukio hilo la mwalimu Zachma kujitosa ziwani lilitokea
Juni 24 mwaka huu majira ya mchana wakati mwalimu huyo akisafiri kwa
kutumia kivuko kutoka Kinesi kwenda Musoma mjini.
“Kuna
tukio la mwalimu mmoja wa shule ya msingi Kibumaye aliyejulikana kwa
jina la Nelson Zachma (50) kujitosa majini, na tukio hili lilitokea Juni
24 mwaka huu majira ya mchana wakati akisafiri kuelekea Musoma mjini
akitokea eneo la Kinesi,” Njewike.
Alisema mara baada ya kujitosa majini,
juhudi za uokoaji zilifanywa na wapiga mbizi wa kivuko hicho lakini
hazikuzaa matunda ndipo marehemu alipozama ndani ya maji na mwili wake
kuopolewa siku tatu baadaye yaani Juni 30 katika mtaa wa Rebu Tarime.
Alisema sababu za mwalimu huyo kuchukua
uamuzi wa kujitosa majini hazijajulikana na polisi bado wanaendelea na
uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini nini chanzo cha mwalimu huyo kuamua
kujiua.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo
aliyejulikana kwa jina la Lucia Kibacho (40) alisema kuwa walipofika
katikati ya kivuko, Zachma alimpatia namba za simu za ndugu zake na
kumwomba awapatie taarifa zake na ndipo akajirusha ndani ya maji.
“Mimi
nilikuwa nimekaa karibu naye, tulipofika katikati ya ziwa, akaniambia
chukua hizi namba ni za ndugu zangu uwajulishe kuwa mimi nimejitosa
majini na nimekufa, mara akajirusha majini,” Kibacho.
Lakini taarifa za awali zinaonesha kuwa,
baadhi ya waombolezaji waliokuwa nyumbani kwa marehemu walisikika
wakisema kuwa Zachma alikuwa na mgogoro wa ndani na mke wake na huenda
ikawa ni moja ya sababu za yeye kuchukua uamuzi huo.


Note: Only a member of this blog may post a comment.