Sunday, July 12, 2015

Anonymous

MPASUKO CCM!

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema kuwa kitendo cha makada watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adamu Kimbisa, kueleza kuwa, hawakubaliani na maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu ni kiashirio kuwa, CCM imeyumba na ina mpasuko ndani yake.

Mchambuzi wa Siasa na Uongozi, Rutashobya Rutashobya, akizungumza na NIPASHE Jumapili jana alisema kuwa kitendo cha makada hao juzi usiku kuibuka na kauli moja kuwa, hawakubaliani na maamuzi yaliyofanyika maana yake wamekosa umuvilivu wa kisiasa na kusababisha chama kuyumba.

Juzi makada hao baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu, waliwaeleza waandishi wa habari kuwa, hawakubaliani na maamuzi yaliyofanywa na kikao hicho ya kuminya baadhi ya majina ya wagombea.

Aidha, walisema kuwa wameletewa majina machache yaliyojadiliwa na Kamati ya Maadili, kitendo ambacho hawakukubaliana nacho kwa mujibu wa Katiba ya chama.

Nchimbi na wenzake walisema tayari wameshawataarifu wenzao kuhusiana na maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu ya kutounga mkono kile kilichotokea.

Akizungumzia maamuzi hayo, Rutashobya, alisema , makada hao walitakiwa kuwa na uvumilivu wa kisiasa lakini walichokifanya inaonyesha dhahiri kuwa kuna mpasuko na chama kimeyumba.

Aidha, alisema kwa wale walioenguliwa kwa bahati mbaya sababu hazijawekwa wazi hivyo ni vigumu kama wachambuzi kuchambua kitaalam.

Aidha alisema bado wananchi wana nafasi kubwa ya kuchagua Rais ajae.
Akielezea kuhusu kuenguliwa kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye mikutano yake wakati akitafuta udhamini ilifurika wananchi, alisema inawezekana waliokuwa wakijitokeza walikuwa wanapenda kitu kingine cha ziada na sio mhusika.

“Mtu aliyekuwa anajaza umati mkubwa uwanjani leo ameenguliwa lakini nchi ipo shwari hakuna aliyeenda barabarani kufanya maandamano kupinga maamuzi, ni tafsiri kuwa labda umati ule ulikuwa ukienda pale kushangaa waimbaji, magari na sio upendo wa dhati kwa mhusika,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) Bashiru Ally, alisema kama mchambuzi wa siasa, kilichotokea na kitachotokea atakichambua kwa kina kwa faida ya Watanzania.

Alisema endapo leo jina la mgombea litatoka basi atakuwa na uwanja mpana wa kuchambua mchakato mzima kutoka watia nia 42 hadi wakabaki 38 na mwishoe watano.

Kuhusu kuenguliwa kwa Lowassa na watia nia wengine alisema anaamini maswali yanayoulizwa nje na wananchi hata ndani ya vikao yapo.

“Huu ni mwanzo tu kwa yaliyotokea nafikiri yapo matokeo kama 1000 yataweza kutokea lakini sasa ni mapema mno kuchambua tuvute subira hadi jina la mgombea urais litakapotoka,” alisema.

Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, Alexander Makulilo, alisema kilichotokea kwa CCM inaonyesha kuwa, kuna shida labda Kamati ya Maadili ilipeleka Kamati Kuu majina kama muhuri wa kupitishwa majina badala ya kufanyiwa kazi.

Akitoa maoni kuhusu tano bora, alisema miongoni mwao atakayechaguliwa akipata mfumo mzuri wa uongozi mambo yataenda vizuri.

Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kuenguliwa kwa mtu ambaye alikuwa anaonekana ana nguvu kubwa kwa wananchi ni kiashirio tosha kuwa kazi ndani ya CCM haikufanyika kwa vigezo.

kadhalika kuhusu kitendo cha baadhi ya makada kutangaza kuwa hawana imani na kilichotokea, alisema “Hata kama walifanya mchujo huu naamini CCM ina watu wenye busara na hekima kwa hiyo walipaswa kuwa na maridhiano,” alisema.

Aliongeza kuwa kiashiria cha kilichotokea ni kwamba uchaguzi mkuu utakuwa na makundi yanayopingana ndani ya chama na kuleta fursa kwa upinzani.

Alisema kuwa inapotokea chama kinamkataa mgombea mwenye watu wengi nje anaweza kwenda upinzani na kuzigawa kura.

Aidha, alikitaka chama tawala kujitathmini upya kupitia kile kilichotokea cha baadhi ya wajumbe kupinga maamuzi.
“CCM iangalie upya kanuni zake ili hapo baadaye watu waweze kuhoji maamuzi inapobidi,” alisema.

-NIPASHE

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.