Sunday, July 12, 2015

Anonymous

Wazee wa CCM Walivyoinusuru NEC

Marais wastaafu watatu na makamu wa zamani wa CCM jana walifanya kazi kubwa ya kukinusuru chama hicho kuingia kwenye mgogoro uliokuwa unanukia baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuenguliwa kwenye mbio za urais. 

Kwa mara ya kwanza, wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya chama hicho juzi walijitokeza hadharani na kupinga uamuzi wa chombo hicho wa kupitisha majina ya wagombea kwa njia ambazo walisema zinazokiuka katiba ya CCM. 

Kama hiyo haitoshi, jana wajumbe wa Halmashauri Kuu walimuweka mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete kwenye hali ngumu baada ya kuimba wimbo wa kuonyesha kuwa na imani na Lowassa, likiwa ni tukio la kwanza la aina yake kwenye vikao vya juu vya chama na ambalo liliashiria kuanza kupoteza utii kwa chama. 

Habari kutoka ndani ya NEC zinasema kuwa baada ya mapumziko ya chakula cha mchana, kikao hicho kilijadili kwa kirefu sakata la kuchujwa kwa Lowassa na pande zinazohusika zilizungumza kwa hisia kali, ndipo marais hao, Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi, Abeid Amani Karume na makamu mwenyekiti wa zamani, John Samuel Malecela walipolazimika kuingilia kati.
“Ilibidi kwanza wote waliokuwa wanagombea urais waondolewe kwenye mkutano ndipo tuanze kujadiliana,” alisema mmoja wa wagombea ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe. 

Mjumbe mwingine wa kikao hicho alisema Malecela, Mkapa, Karume na Mwinyi walitumia maneno ya busara na kuwatahadharisha wajumbe dhidi ya misimamo yao.
“Walituonya kuhusu kujali masuala yetu binafsi kuliko amani ya nchi na kututaka kuangalia sana misimamo yetu kwa kuwa inaweza kuhatarisha amani,” alisema mjumbe huyo. 

Alisema wakati kikao kilipositishwa kwa ajili ya chakula cha mchana, kuna baadhi ya wajumbe waliondoka eneo hilo na wengine kubaki, akiwamo Lowassa ambaye hakujulikana alielekea eneo gani kwenye jengo hilo. 

Kikao cha mchana kilianza bila ya Lowassa kuwamo na Karume alianza kuzungumza, na kufuatiwa na Malecela, Mkapa, na Mwinyi, ambaye alipomaliza aliwashauri wajumbe kuwa waendelee na upigaji kura kwa kuwa suala hilo limeshaeleweka.
Mkutano ulipoanza kupiga kura ndipo Lowassa alipoingia na kukuta kazi ya upigaji kura inaendelea na hivyo kuendelea na shughuli hiyo. 

Awali, kwa mara ya kwanza, Kikwete jana alikumbana na mapokezi ya aina yake wakati wajumbe walipomuonyesha waziwazi kupinga uamuzi wa Kamati Kuu kwa kuimba wimbo wa kumuunga mkono Edward Lowassa kabla ya kikao cha Halmashauri Kuu kuanza. 

Hali hiyo imetokea wakati baadhi ya wanachama wa CCM wakiwa bado hawajakubali kuenguliwa kwa Lowassa kwenye kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya CCM baada ya Kamati Kuu kupitisha majina ya John Pombe Magufuli, Amina Salum Ali, Bernard Membe, January Makamba na Dk Asha Rose Migiro kwa ajili ya kupigiwa kura Halmashauri Kuu.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.