Watu wasiofahamika wamesambaza
vipeperushi Zanzibar kupinga maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM kuwakataa
wanasiasa wakongwe waliojitokeza kuwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania akiwemo Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilali na Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa.
Vipeperushi hivyo vyenye kurasa mbili
vimeonekana katika maeneo tofauti vikiwa na kichwa cha habari “Sauti ya
salama Zanzibar”, vimeeleza kuwa kutokana na maamuzi hayo wanachama wa
CCM wa kundi la sauti ya salama kuanzia leo ndio mwisho wa wanachama wa
sauti ya salama kuendelea kubakia ndani ya CCM.
Walisema kundi hilo linaundwa na mikoa
sita ya kichama, wamefikia uamuzi huo baada ya kuridhishwa na utaratibu
mzima wa upatikanaji wa mgombea wa nafasi ya urais kutokana na chama
kushindwa kupitisha mgombea ambaye ni chaguo la wananchi na wanachama.
“Kama
mtatuletea mgombea wenu wa mfukoni badala ya Lowassa ambaye ndio chaguo
la wanachama wengi na wananchi, Jumapili ndio mwisho kwa wanachama wa
sauti ya salama kuendelea kubakia ndani ya CCM”, vimeonya vipeperushi hivyo.
Aidha, kundi hilo limesema wajumbe wa
halmashauri kuu ndio wanaowategemewa na kama watashindwa kukiokoa chama
kwa kushindwa kuwapatia wanachotaka, wanachama historia itakuja
kuwahukumu kama ilivyotokea kwa vyama vya ukombozi katika mataifa ya
Malawi, Zambia na Kenya baada ya vyama husika kushindwa kuheshimu
demokrasia ya ndani ya chama.
Kundi hilo limesema kuwa kumbukumbu
inaonyesha mchakato wa kupata mgombea wa urais CCM umekuwa ukimalizika
na kuacha nyufa ndani ya chama kama ilivyotokea mwaka 2000 baada ya
wananchama na wananchi wa Zanzibar kumtaka aliyekuwa Waziri Kiongozi,
Dk. Mohammed Gharibu Bilali awe mrithi wa rais mstaafu Dk Salmin Amour,
baada ya kumaliza muda wake.
Vipeperushi hivyo ambavyo vimeibua
mjadala vimeeleza kwamba mwaka 2010 chama kiliendelea kurejea makosa
yale yale kuchagua mgombea wa mfukoni badala ya yule aliyetakiwa na
wananchi ambao walikuwa wakimtaka Dk. Bilal na badala yake aliletwa
mgombea Dk Ali Mohammed Shein na kusababisha CCM kushinda kwa asilimia
51.
“Kamati kuu, halmashauri kuu pamoja na
mkutano mkuu kama utashindwa kusoma alama za nyakati tutalazimika
wanachama kupita njia yenye usalama na miguu yetu, kumbukeni vipo vyama
vingi na tayari Chadema imetuonesha njia”.


Note: Only a member of this blog may post a comment.