Sunday, July 12, 2015

Anonymous

Messi atia doa urafiki wa SIMBA SC, AZAM FC


Ramadhan Singano 'Messi'
Dar es Salaam. Usajili wa Ramadhan Singano ‘Messi’ kutoka Simba kwenda Azam kwa mkataba wa miaka miwili umeanza kuibua hisia za ushindani na uhasama mkubwa baina ya timu hizo mbili, ambazo awali zilidhaniwa na wengi kuwa ndugu.

Kwa mtazamo wa wadau na wachambuzi mbalimbali wa michezo nchini, uhasama huo utaweza kukuza kiwango cha soka kwa klabu hizo mbili, endapo utatumiwa vizuri.

Udugu ambao umekuwapo baina ya Simba na Azam, kwa mtazamo wa viongozi wa Simba umeingia doa, kiasi cha kumeguka na kuwafanya mashabiki wake kuanza kufikiria hisia za ushindani baina ya Simba, Azam, kuliko ilivyokuwa misimu michache iliyotangulia.

Awali, Simba na Azam zilitajwa kuwa na udugu kwa maelezo kuwa mashabiki wengi wa Azam na baadhi ya viongozi wao waliaminika kuwa ni wapenzi na mashabiki wakubwa wa Simba, lakini sasa mambo yanavyokwenda, undugu baina yao unakaribia mwisho.

Mgogoro na hatimaye usajili wa ‘Messi’ aliyejiunga na Azam siku mbili zilizopita umeibua hisia za uhasama zaidi ya urafiki baina ya klabu hizo mbili.

Messi ametua Azam kwa mkataba wa miaka miwili baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kubariki kuvunjwa kwa mkataba baina yake na klabu yake, Simba.

Hata hivyo, uamuzi huo unaelekea kuwaudhi baadhi ya viongozi wa Wekundu wa Msimbazi, ambao kwa sasa wameibuka na kuanzisha vita mpya ambayo pengine itaifanya mechi baina ya timu hizo msimu ujao kuwa zenye ushindani mkali kuliko miaka ya nyuma.

Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe alisema juzi kuwa Azam ilihusika kwenye kumshawishi mchezaji huyo hadi ikafikia kutua Azam.

Hanspoppe alisema kuanzia sasa, atawashauri wanachama wa Simba kutonunua bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na Kampuni ya Azam kwa madai kuwa wamefanya uhuni na hila dhidi yao kwa kumshawishi na kumsajili mchezaji wao.

Hanspoppe alidai kuwa kuendelea kununua bidhaa hizo ni kuwapa nguvu wapinzani wao wakati wao wanawadhulumu.

Awali, Azam na Yanga ndizo zilizooenekana kuwa na uhasama wa muda mrefu tangu mwaka 2012, lakini kwa sasa uhasama huo umepoa kama ilivyoshuhudiwa kwenye mechi za mwishoni mwa msimu uliopita.

Wakati ule, Azam walionekana kuomba huruma kwa Yanga ili ilegezewe katika mechi yao waliyokutana ili wapate nafasi ya pili ya kushiriki michezo ya kimataifa.

Tayari, Yanga iliyokuwa imetwaa ubingwa ilipokutana na Azam inadaiwa kucheza bila kuonyesha ushindani wa dhati, kwa sababu wao ambao ni watani wa jadi wa Simba, hawakutaka wapinzani wao, Wekundu wa Msimbazi wapate nafasi ya pili, hivyo wakaona liwalo na liwe ni bora wamalize uhasama na Azam kwa kuwapa ushindi katika mechi ilimradi tu Simba asipate hiyo nafasi.

Yanga ilikuwa na uhasama na Azam tangu timu hizo zilipokutana Machi 10, 2012 katika mchezo wa Ligi Kuu, ambao Azam ilishinda 3-1, huku baadhi ya wachezaji wa Yanga wakidaiwa kumpiga mwamuzi Israel Nkongo kwa madai kwamba alikuwa akiwabeba wapinzani wao.

Baada ya mchezo huo, TFF iliwafungia wachezaji watano wa Yanga, jambo lililoibua hasira kwa viongozi wa timu hiyo na mashabiki wao na ndipo chuki zilipoibuka dhidi Azam kila mara walipokutana uwanjani.

Wachezaji waliofungiwa ni, Stephano Mwasyika, mwaka mmoja na faini ya Sh1 milioni moja, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, mechi sita na faini ya Sh500,000, Nurdin Bakari, mechi tatu na faini ya Sh500,000, Omega Seme mechi tatu na faini ya Sh500,000 na Jerryson Tegete miezi sita na faini ya Sh500,000.

Pia, Yanga ilipigwa faini ya Sh1 milioni baada ya mashabiki wake kufanya vurugu na timu hiyo kuonyeshwa kadi tano kwenye mechi hiyo.

Uhasama kwa timu hizo ulikolezwa zaidi na mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji aliyeigomea Kampuni ya Azam Media kuonyesha laivu mechi za Ligi Kuu Bara za timu hiyo, huku pia akigomea udhamini wa Sh100 milioni uliotolewa kwa ajili ya kurushwa kwa matangazo ya mechi hizo.

Kauli hiyo ya Hanspoppe imeonyesha kuwa mambo yamegeuka na inaonekana vita baridi imeibuka baina ya Simba na Azam, jambo linalomaanisha kuwa msimu ujao mechi baina ya timu hizo mbili itakuwa yenye ushindani mkubwa.

Hanspoppe na viongozi wenzake Simba wanailalamikia Azam kuwa ndiyo iliyomshawishi mchezaji huyo (Messi) alalamike TFF kuwa hana mkataba na klabu hiyo ili iwe rahisi wao kumchukua.

Juzi, Simba iliijia juu Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya TFF kwa madai kuwa inaendeshwa kishabiki zaidi badala ya kuzingatia sheria na taratibu na uamuzi wa kamati hiyo ulitolewa kwa shinikizo kutoka upande fulani.

Mchambuzi wa masuala ya michezo, ambaye pia ni kocha, Joseph Kanakamfumu anasema kuwa anauona uhasama baina ya timu hizo mbili kubwa, huku akieleza kuwa uhasama huo utaleta upinzani mkubwa uwanjani, lakini akazionya klabu hizo kuwa wasiumizane.

“Uhasama unaonekana kwa kiasi kikubwa, ingawa mimi nafurahi kwani uhasama unaleta upinzani uwanjani,hivyo msimu ujao mechi ya Simba na Azam kila mtu atatamani kuiona kuliko ilivyokuwa msimu uliopita,ili mradi wasiuane tu,” alisema Kanakamfumu.

Kocha wa Polisi Tabora, Zulfikar Mahadi kwa upande wake alisema hafikirii kama usajili wa Singano kwenda Azam unaweza kuwa mwisho wa uhusiano uliopo baina ya timu hizo na kuibua uhasama, hivyo kuitaka Simba ilichukulie kama jambo la kawaida katika soka.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.