RAIS Mteule John Pombe Joseph Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi sasa ni full kicheko kufuatia kutangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi mkuu wa urais 2015.
Ushindi wa Dk. Magufuli dhidi ya Lowassa ambaye amelalamika kuchezewa rafu, ulianza kuonesha dalili tangu kuanza kutangazwa kwa matokeo hayo Jumatatu iliyopita, kwani mara zote alikuwa mbele ya mpinzani wake huyo wa karibu.
Mara baada ya kutangazwa ushindi huo, wafuasi wa CCM katika mitaa ya Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake walilipuka kwa furaha, wakipongezana kwa kazi kubwa na ngumu waliyoifanya ndani ya miezi miwili ya kampeni, ambazo kwa mara ya kwanza walikumbana na upinzani mkubwa kuliko chaguzi zote zilizopita.
KUMBE JANA ILIKUWA BETHIDEI YAKE
Katika hali ya kustaajabisha, jana ilikuwa ni siku ya matukio mawili makubwa maishani mwake, kwanza ikiwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa rais huyo mteule, ambaye pia alizaliwa siku kama ya jana, Alhamisi, miaka 56 iliyopita na kutangazwa kuwa kiongozi wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.
“Kuna watu wengine wana bahati zao hapa duniani, yaani mtu leo ni kumbukumbu ya siku yako ya kuzaliwa, halafu unapewa zawadi ya kutangazwa kuwa rais wa nchi, kwa kweli ni jambo kubwa sana, ingawa jukumu alilopewa ni zito, tuna imani atalimudu,” alisema kijana mwingine aliyesema ni mfuasi wa upinzani lakini aliyempigia kura ya urais Magufuli.
MASTAA WAMFUNGUKIA
Mastaa mbalimbali wa muziki na filamu waliokuwa katika timu mbalimbali za kampeni za mgombea huyo wa CCM, walisema waliutarajia ushindi wake, hasa kwa jinsi walivyozunguka nchi nzima kumnadi na wengi kuonekana kumkubali kulingana na historia yake ya utendaji. Unataka kusikia walichokisema kuhusu ushindi wa Magufuli? Nenda ukurasa wa 9.
KUTOKA KWA MHARIRI
Tunachukua nafasi hii kumpongeza Mhe. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano na tunamtakia kila la kheri katika kutimiza majukumu yake.
Note: Only a member of this blog may post a comment.