Kocha wa Simba, Dylan Kerr
Lushoto. Kocha wa Simba, Dylan Kerr amesema anataka wachezaji wote wa timu hiyo wawe wamejiunga na kambi yake iliyoko hapa, la sivyo watafute timu nyingine za kuchezea. Kocha huyo amesisitiza kuwa wachezaji hao ni pamoja na wale waliosajiliwa kujiunga na timu hiyo kwa mara ya kwanza kwani wanachelewesha programu zake.
Wachezaji wa Simba ambao walikuwa hawajajiunga na kambi hiyo hadi jana asubuhi ni nahodha Hassan Isihaha, beki wa kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, viungo Abdi Banda, Said Ndemla na Jonas Mkude.
Wachezaji wapya wa timu hiyo ambao bado hawajafika ni Laudit Mavugo na beki mmoja kutoka nchini Burundi.
“Inabidi wachezaji wote wajiunge nasi wikiendi hii, programu zangu zinachelewa, kama hawatakuja wikiendi hii watafute timu nyingine za kucheza,” alisema Kerr.
“Hii inahusisha wachezaji wapya pia, kama wamesajiliwa tayari wanatakiwa kujiunga na timu.”
Kocha huyo alitumia muda mwingi juzi jioni na jana asubuhi kuwafanyisha wachezaji wake mazoezi ya kufunga kwa kutumia mipira ya krosi na pasi ndefu kutoka katikati ya uwanja.
Kerr aliwataka wachezaji wote kuwa na uwezo huo wa kufunga hata kama wanacheza nafasi za ulinzi ambapo katika mazoezi hayo, Peter Mwalyanzi, Issa Said, Ibrahim Ajibu, Elius Maguri, Michael Mgimwa, Hamis Kiiza na Mohammed Faki walionekana kufanya vizuri zaidi.
Kocha huyo ameamua kuwapa wachezaji wake mapumziko kuanzia jana mchana hadi kesho, Jumatatu asubuhi ndipo wataendelea na mazoezi mengine.
Kocha huyo raia wa Uingereza amewapa wachezaji wake uhuru wa kutalii mjini hapa, lakini amewataka kuwa waangalifu na kusimama katika misingi ya soka.
“Mtakuwa huru baada ya mazoezi haya ya asubuhi, mmefanya kazi kubwa kwa wiki nzima ambayo tumekuwa hapa, mkienda kutembea muwe waangalifu.
“Msifanye vitu vya ajabu mkaharibu kazi tuliyoifanya,hiyo itakuwa mwisho wa uhuru niliowapa,” Kerr aliwaambia wachezaji wake.


Note: Only a member of this blog may post a comment.