Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, jana alikana kutoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwamba mtoto, hana akili na mpuuzi.
Askofu Gwajima alikanusha tuhuma hizo wakati akisomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilfred Dyansobera anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo,
alidai kuwa kati ya Machi 16 na 25, mwaka huu katika viwanja vya
Tanganyika Packers, vilivyopo Kawe jijini Dar es Salaam, mshtakiwa
alitoa lugha ya matusi kwamba ‘mimi
Askofu Gwajima nasema askofu Pengo ni mpuuzi mmoja yule, mjinga mmoja,
amekula nini yule, sijui amekula nini yule mtoto hana akili yule’ alinukuu maneno hayo.
Alidai kuwa Askofu Gwajima alitoa maneno
hayo yakufadhaisha dhidi ya Askofu Pengo na kwamba yanaweza kusababisha
uvunjifu wa amani.
Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa Machi
27, mwaka huu mshtakiwa alifikishwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar
es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa.
Ilidaiwa kuwa alifunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani dhidi ya tuhuma hizo.
Hata hivyo, Askofu Gwajima alikana
mashitaka hayo lakini alikiri majina yake, wadhifa wake, kuhojiwa Kituo
cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kweli kanisa lake liko Kawe na
kushitakiwa mahakamani hapo.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa unatarajia kuita mashahidi saba na watawasilisha vielelezo vitano.
Wakati huo huo, mahakama hiyo imepiga
kalenda kusoma maelezo ya awali ya kesi inayomkabili askofu huyo na
wenzake watatu, baada ya mshtakiwa wa nne kuwa mgonjwa.
Kesi hiyo itasikilizwa mbele ya Hakimu Dyansobela Agosti 10, mwaka huu.
Note: Only a member of this blog may post a comment.