Friday, July 3, 2015

Anonymous

LAZIMA WAKAE! Mazoezi ya Mzungu SIMBA SC ni Balaa!

Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr.
Wilbert Molandi, Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Simba, Dylan Kerr, ameanza kwa kasi majukumu ya kuinoa timu hiyo ambapo jambo la kwanza alilouliza ni kwa nini timu hiyo imeshindwa kutwaa ubingwa kwa misimu mitatu mfululizo!

Akiwa hajapata jibu la kumridhisha, akaamua kuanza mafunzo ya kiwango cha juu kwa kuonyesha wazi anataka kuzima utawala wa Azam FC na Yanga ambao wamekuwa wakipokezana ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Akisimamia mazoezi ya timu yake kwa siku ya pili katika Uwanja wa TCC Chang’ombe jijini Dar, jana na juzi, gazeti hili lilibaini mambo kadhaa yakiwemo ambayo ameyazungumza yeye mwenyewe:

Soka la pasi
Katika mazoezi hayo, Kerr alionekana kusisitiza soka la pasi muda mwingi, tena za haraka ambapo alisema anaamini hiyo ndiyo njia pekee ya kuwavuruga wapinzani wakati wa mechi.

Programu hiyo pia iliwashirikisha makipa wa timu hiyo pamoja na wachezaji wengine wote wa ndani huku Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola naye akionekana kuwa bega kwa bega.

Kontroo nyingi
Kerr alionekana kuweka msisitizo kwenye umiliki wa mpira huku akisisitiza wachezaji kuwa na uwezo mkubwa wa kupiga ‘kontroo’.

Mashambulizi ya kushtukiza
“Mfumo wangu ninaoutaka katika soka ni kufanya mashambulizi ya kushtukiza, lengo la kuwapa mafunzo hayo ni ushindi pindi tunapokutana na wapinzani wasumbufu na siyo kuishia kupiga pasi nyingi pekee.

Ubingwa
“Baada ya hivyo vyote kuvimaliza kwenye programu zangu, nguvu zangu nitazielekeza kwenye ubingwa wa ligi kuu msimu ujao.

“Nimepewa taarifa na viongozi wa Simba juu ya timu kushindwa kuchukua ubingwa kwa kipindi cha miaka mitatu, ninapenda kuwaahidi mashabiki wa Simba ubingwa, lakini hilo halitawezekana bila ya kuwa na wachezaji wazuri.

Aomba mechi nne ngumu
“Baada ya kumaliza programu zote, nimeomba tupatiwe mechi nne za kirafiki kwa ajili ya kuona kile tulichojifunza mazoezini kama kimefanyiwa kazi.

Apewa video nane za Yanga
“Yanga ni wapinzani na watani wetu, nimepata taarifa zao lakini siwajui vizuri, hivyo ninahitaji kuwaona zaidi kwa kuziangalia mechi ambazo wamecheza.“Nilibahatika kuwaona walipocheza na SC Villa ya Uganda kipindi kimoja, nilichelewa kufika uwanjani kutokana na foleni.

“Nimewaomba viongozi wanitafutie video nane za Yanga walizocheza msimu uliopita, nikizipata nitajua vitu vingi kuhusu wao ikiwemo mfumo, wachezaji wenye madhara na mengine mengi,” alisema Kerr, mwenye daraja A na B la ukocha ya Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa). Wakati huohuo, Kerr alisema uwanja wanaoutumia kwa mazoezi siyo mzuri na haufai kwa mazoezi ya kiufundi. “Uwanja siyo mbaya sana, ni mzuri kidogo lakini haufai kwa ajili ya mazoezi ya kiufundi, uwanja huo unafaa kwa ajili ya kukimbilia na viungo pekee,” alisema.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.