Monday, July 13, 2015

Anonymous

MAVUGO: Nitaliziba Pengo la OKWI

Laudit Mavugo.
Na Mohammed Mdose, Dar es Salaam
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Burundi, anayetarajiwa kutua Simba hivi karibuni, Laudit MavugoA, amewasisitiza viongozi wa timu hiyo kufanya haraka kukamilisha dili lake la usajili huku akiwahakikishia kuwa, ataliziba vilivyo pengo lililoachwa na mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi.

Dili la Mavugo kutua Simba limeshakamilika nusu kwani tayari Simba wameshafanya mazungumzo na mshambuliaji huyo na kukubaliana kila kitu ila ugumu upo kwa uongozi wa klabu yake ya Vital’O ambayo ndiyo inalichelewesha dili hilo kwani kuna vitu bado hawajakubaliana na uongozi wa Simba.

Akizungumza na Championi Jumatatu moja kwa moja kutoka Bujumbura, Burundi, Mavugo alisema kuwa iwapo atatua Simba, viongozi na mashabiki wa timu hiyo wajue kabisa watamsahau Okwi kwani atafanya vitu vikubwa.

Alisema kuwa awali alikuwa anapiga hesabu za kucheza pamoja na Mganda huyo lakini baada ya kupata taarifa za kuondoka, anajipanga kuja kuliziba pengo lake kwani hicho ndicho kwa sasa kinahitajika kwenye timu hiyo.

Aliweka wazi kuwa amefikia hatua hiyo ya kuwa na uhakika wa kuliziba pengo hilo kwa kuwa alishawahi kufanya hivyo kipindi, Amissi Tambwe anaondoka Vital’O kuja Simba, yeye alipewa jukumu la kuliziba pengo lake na akafanya hivyo hadi kuwa mfungaji bora msimu uliopita akitupia mabao 32 katika mechi 30 alizocheza.

“Okwi ameondoka? Inaniuma sana, nilidhani tutakuwa wote tukishirikiana, ila nitaweza kuliziba pengo lake kwani nakumbuka wakati Tambwe yupo Vital’O alikuwa mfungaji bora mara tatu, kipindi alipokuwa anaondoka nilitakiwa nizibe pengo lake na nikafanya hivyo,” alisema Mavugo.

Kocha Dylan Kerr amemwambia mwandishi wetu, Omar Mdose mjini Lushoto kuwa, anaamini Mavugo atawasaidia sana.
“Kama unavyojua huku tukiwa tunaendelea na mazoezi bado wachezaji wengine hawajawasili lakini naamini Jumatatu (leo) tutakuwa nao pamoja.

“Lakini pia nasubiri akija huyo Mrundi (Mavugo) basi atakuwa msaada mkubwa kwenye kikosi chetu licha ya kwamba kwa sasa mastraika wapo lakini na yeye ataongeza nguvu kwenye safu hiyo,” alisema Kerr.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.