NIAlhamisi
tena ambayo huwa nakutana na nyie wasomaji wangu ninaowapenda sana.Leo
nataka kuzungumza na wanandoa. Ndiyo maana nimeanza kwa kusema hapo juu
kuwa, ndoa isishikiliwe kama gauni la harusi.
Katika ndoa kuna raha na karaha au shida. Kumbuka kuwa wewe mwanandoa
uliapa utaishi na mwenzako katika maisha yote. Hicho kiapo ulikitoa
kanisani au msikitini tena kwa kuulizwa mara tatu.
Ndoa ni daraja. Kama zima unatakiwa kulivuka kama bovu pia unatakiwa
kulivuka. Lakini kama ni bovu lifanyie ukarabati kwa sababu unatakiwa
kuvuka.Kama nilivyoongea, katika ndoa kuna misukosuko kama lilivyo
daraja bovu. Ni jukumu lako mwanandoa kuhakikisha unavuka. Ndani ya ndoa
kuna vikwazo vingi, kukosa kupo, kupata ni hali ya kawaida ambayo ipo
na lazima ukabiliane nayo kama ulivyoahidi siku uliyofunga ndoa.
KWA WANAWAKE WENZANGU
Kuna baadhi ya wanawake pale waume zao wanapokosa cha kusababisha
uhai uendelee, basi hadi mtaa wa saba watapata taarifa. Kumbuka hakuna
mkamilifu isipokuwa Mwenyezi Mungu tu. Wewe mke uwe mstari wa mbele
kuujua udhaifu wa mumeo kama vipi muweke chini mumeo mweleze, muongee
kwa upole kabisa. Kumbuka wewe ndiyo hakimu wa nyumba yako, wewe ndiyo
waziri. Unayo madaraka yote juu ya familia na mumeo kwa ujumla.
KWA WANAUME NAO
Na
wewe mwanaume vilevile, ukigombana na mkeo haitakiwi siri itoke nje.
Muweke kikao, mseme uwezavyo kisha myamalize. Nasema hivi kwa sababu
wale unaowapelekea mashitaka, baadhi yao wana ushauri mzuri, lakini
wengine ushauri wao ni mbaya hata kushauri ndoa ivunjike.
TABIA ZA WATU
Leo utachukua tatizo la mumeo unampelekea shoga. Kumbe huyohuyo shoga
anamtaka mumeo. Na wewe mwanaume vilevile, utapeleka tatizo la ndoa
yako kwa marafiki zako kumbe na wao wanampenda mkeo, walianza kumtamani
tangu walipomuona siku ya kwanza unamuoa. Je, mtakuwa mnajenga kweli au
mnajibomoa?
CHA KUFANYA
Kama kuna matatizo katika ndoa yenu, kaeni wenyewe ndani hata bila
watoto kujua mmegombana myamalize kwa ajili ya kulinda ndoa yenu. Kuna
wanandoa wengine hupenda kupeleka migogoro yao kwa watu wazima. Je,
hamjui kama siku hizi hata watu wazima wanapenda serengeti boi? Shauri
yenu!
Ndiyo maana nikasema kuwa usimpe tatizo mtu ambaye kesho na
keshokutwa atakushushia hadhi na heshima yako. Hii ina maana ya kichwa
cha habari kuwa ndoa usiigeuze gauni la harusi ambalo hushikiliwa na
wapambe, liache liburuzike lenyewe ikibidi libebe mwenyewe.
Thursday, July 9, 2015
JAMANI! NDOA ISISHIKILIWE KAMA GAUNI LA HARUSI!
USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK
TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)
Filed Under:
MAPENZI
on Thursday, July 9, 2015

Note: Only a member of this blog may post a comment.