Ugonjwa wa Trich ni ugonjwa
unaosababishwa na vimelea vya jamii ya Protozoan na huathiri mrija wa
kupitisha mkojo unaojulikana kama Urethra na tupu ya mwanamke (vagina).
Ugonjwa huu huwapata pia wanaume lakini
huonekana zaidi kwa wanawake na daktari anaweza kumuambia mgonjwa
anayeugua maradhi haya kuwa ana Trichomonas vaginalis.
Kwa upande wa wanaume wanaweza kuuepuka
ugonjwa huu kutokana na kuwa na majimaji ya kwenye tezi dume na madini
ya Zinc ambayo huathiri vimelea vinavyosababisha ugonjwa huu,
vinavyoitwa Trichomonas Vaginalis.
UNAAMBUKIZWAJE?
Mwanamke au hata mwanaume anaweza kukumbwa na ugonjwa huu akifanya tendo la ndoa na mtu mwenye maambukizi bila kutumia kinga.
Kwa kawaida vimelea vya Trichomonas
Vaginalis ni vidogo mno ni sawa na chembechembe moja ya damu nyeupe kwa
upana (10 μm) ingawa wakati mwingine ukubwa waweza kutofautiana
kulingana na mazingira. Wengine huuita ugonjwa huu Trichomoniasis.
Watu wenye Trich wana hatari ya kupata
ugonjwa wa Ukimwi (HIV) au magonjwa mengine ya zinaa kwa sababu bakteria
hawa huharibu seli aina ya Epithelium na kusababisha vidonda
(Microulcerations) katika tishu zilizo ndani ya utupu wa mwakamke.
DALILI KWA WANAWAKE
Dalili za Trich huanza kuonekana kuanzia
siku ya 4 mpaka ya 28 baada ya mtu kupata maambukizi ya ugonjwa huu.
Kwa wanawake, Trich huathiri shingo ya kizazi (Cervix), mrija wa mkojo,
tupu ya mwanamke, kibofu cha mkojo, tezi zinazojulikana kama Bartholin
Glands na Skene Glands.–
Wanawake waliokumbwa na ugonjwa huu
hutokwa na uchafu sehemu zao za siri na huwa na rangi ya njano, kijani
au kijivu na huwa mzito. Dalili nyingine ni kuwa na maumivu wakati wa
kujamiiana na kutoka harufu mbaya.
Mgonjwa pia hujisikia maumivu wakati wa
kujisaidia haja ndogo na shingo ya kizazi huwa nyekundu lakini hili
ataligundua daktari akifanya uchunguzi kwa mgonjwa.
Dalili nyingine ni kuwasha sehemu za
siri, kupata maumivu chini ya kitovu.Wanawake wengine wanaweza kuwa na
vimelea hivi na wakaishi navyo kwa mwaka mzima bila kugundua kama
hawatakwenda kupimwa.
DALILI KWA WANAUME
Kwa upande wa wanaume, vimelea hivi vya
ugonjwa huu hupatikana katika sehemu za siri nje ya mrija wa kupitisha
mkojo yaani anterior urethra, kwenye tezi dume yaani prostate na
kwenye mirija ya kuhifadhi na kutoa mbegu za kiume kitaalamu huitwa
epididymis.
Waliokumbwa na maradhi haya wanaweza
kupata dalili hizi: Kuwasha na kutokwa na uchafu au majimaji kutoka
kwenye uume wake au kuwa na kichomi baada ya kujisaidia haja ndogo au
baada ya kutoa mbegu za kiume.
UGUNDUZI
Mgonjwa hugundulika baada ya kufanyiwa
vipimo. Kipimo cha hadubini (microscope) hutumika ambapo daktari
huingiza kifaa maalum katika tupu ya mwanamke kinachojulikana kama
speculum na kuchukua kipimo kwa kutumia pamba maalum (cotton swab) na
kupeleka maabara kuangalia kama kuna vimelea vya trichomonas vaginalis.
Daktari pia anaweza kuangalia kama kuta
za ndani za tupu ya mwanamke au shingo ya kizazi zimeathirika kwa kuwa
na vidonda ambavyo ni vyekundu.
Wanaume pia huchunguzwa kwa kuchukuliwa
uchafu unaotoka kwenye uume wake kwa kutumia pamba (Cotton swab) kisha
kupeleka maabara kufanyia uchunguzi kwa kuoteshwa kwenye maabara
kitaalamu huitwa culture, kuangalia kama kutakuwa na uoto wa vimelea vya
ugonjwa huu baada ya siku tatu.
Mwanamke pia anaweza kuchunguzwa kama
ana kiwango cha tindikali (PH) kwenye tupu ya mwanamke kwa kutumia
karatasi maalum ya kipimo hiki (PH paper). Magonjwa yanayobadilisha PH
hii ni pamoja na trichomoniasis, bacteria vaginosis, atrophic vaginitis
nk.
Vipimo vya ugonjwa huu ni vingi kama
vile kipimo cha damu kuchunguza Prostate Specific Antigen (PSA): PSA ni
aina ya protini inayozalishwa na seli za tezi dume. Kipimo cha Pap
smear ambacho hupima chembechembe au seli za shingo ya kizazi ambazo
huchukuliwa na kuchunguzwa kutumia darubini. Kipimo hiki pia hutumiwa
katika uchunguzi wa wanawake ili kujua kama wamepata HYPERLINK
“http://tanzmed.com/index.php?option=com_k2&view=item&id=75:saratani-ya-shingo-ya-kizazi-cervical-cancer&Itemid=160”saratani
ya shingo ya kizazi au la.
Kuna kipimo kingine kinachoitwa Elisa
for HIV ambacho huangalia maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi, kipimo cha
mkojo, cha damu, na kadhalika.
Tiba na ushauri
Tiba ya ugonjwa huu ni kutumia dawa aina
ya metronidazole au flagyl. Kwa wanawake wenye ujauzito wa chini ya
miezi mitatu wasitumie dawa hii na hata wale ambao wananyonyesha, badala
yake wamuone daktari.
Wale walioathirika, wanashauriwa kupata
tiba pamoja na wenza wao. Dawa hizi zina madhara mbalimbali kama vile
dawa ya metronidazole ambapo mgonjwa huweza kupata mzio (allergic
reaction), kichefuchefu, kukauka midomo, kuharisha, kushuka kiwango cha
chembechembe nyeupe za damu (leukopenia) ambazo hutoa kinga dhidi ya
magonjwa mbalimbali na hivyo kumuweka mtu kwenye hatari ya kupata
maambukizi ya maradhi.
Wanawake wenye zaidi ya miaka 18 au wale wenye upungufu wa kinga mwilini wanashauriwa kufanya vipimo hivi kila mwaka mara moja.
Mgonjwa asipotibiwa mapema, anaweza
kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi akijamiiana na mtu mwenye
maambukizi na kwa wanawake huwasababishia kuzaa watoto njiti au wenye
uzito mdogo na wanaweza kupata saratani ya shingo ya kizazi na wanaume
wanaweza kukumbwa na saratani ya tezi dume.
Itaendelea wiki ijayo
Note: Only a member of this blog may post a comment.