Amissi Tambwe
Nassor Gallu,Dar es SalaamUMEISIKIA HII? Uongozi wa Yanga una jeuri baada ya kuamua kuweka wazi kuwa klabu yoyote yenye jeuri ya fedha ya kuweza kumnyakua mshambuliaji wao, Mrundi, Amissi Tambwe, basi inakaribishwa.
Uongozi huo umetamka kuwa wachezaji mahiri wa kikosi hicho akiwemo Tambwe, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima na mfungaji bora wa msimu uliopita, Simon Msuva, wapo sokoni na kama kuna klabu yoyote inawataka, inaweza kuwauzia kama watafikia makubaliano kwa kuwa soka ni biashara na wachezaji wao ni kama bidhaa.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, aliyasema hayo baada ya kuulizwa kisa cha kumuachia aliyekuwa kiungo mahiri wa timu hiyo, Mrisho Ngassa, kujiunga na Klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini kwa mkataba wa miaka minne wakati bado ana uwezo mkubwa.
Akizungumzia ishu hiyo wakati Yanga wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume, Tiboroha alifafanua kuwa si Ngassa pekee, bali mchezaji yeyote aliyemo katika kikosi hicho anauzwa, ingawa kila mchezaji ana bei yake kulingana na kiwango chake kwa muda husika.
“Sisi Yanga tunachukulia soka kama biashara yoyote na wachezaji ndiyo bidhaa yetu. Kwa hiyo siyo Ngassa tu kuondoka Yanga, mchezaji yeyote hapa anaweza kuuzwa muda wowote kama klabu inayomtaka itafikia makubaliano na sisi. Hili suala lipo dunia nzima, mchezaji anaweza kuwa nguzo katika timu lakini akaondoka na klabu husika ikaingiza kipato na kutafuta mbadala wake.
“Kinachozingatiwa ni kufuata utaratibu sahihi, kila mchezaji ana thamani yake kutokana na uwezo alionao kwa muda husika. Kwa hiyo timu ikimuona mchezaji anawafaa sisi tunamuuza tukifikia makubaliano,” alisema Tiboroha ambaye aliwahi kuwa kiongozi katika Klabu ya Malmo FF ya Sweden.

Note: Only a member of this blog may post a comment.