
Afisa Afya kata Nyasubi Mkola Vedastus (27) mkazi wa Nyahanga wilayani Kahama akiwa katika kituo cha afya cha Igalilimi Kahama
Akizungumza na wandishi wa Habari Vedastus waliomtembelea katika kituo cha Afya cha Igalilimi mjini Kahama alipolazwa akipatiwa matibabu amesema tukio hilo limetokea juzi saa kumi jioni wakati anatoka bafuni ndipo shemeji yake alipomwagia maji hayo ya maharage.
Vedastus amesema alimwagiwa maji ya maharage yaliyokuwa jikoni yakichemshwa na mke wa kaka yake bi Anna Makula wakati akitoka bafuni kuoga na wakati huo alikuwa amevaa kaushi na taulo.
Amedai kuwa chanzo cha tukio hilo alikuwa na ugomvi wa ndani na shemeji yake ambaye wamepanga nyumba moja katika mtaa huo.
Amesema wakati anakwenda bafuni kuoga alimpita shemeji yake pembeni ya mlango akiongeza maji kwenye maharage wakati huo huo chumbani kwake akiwa amemwacha rafiki yake wa kike ambaye ana mahusiano naye kimapenzi na wakati anarudi ndani ndipo alijikuta akimwagiwa maji hayo na shemeji yake.
Baadhi ya watu waliozungumza na Malunde1 blog wanasema tukio hilo linahusishwa na mahusiano ya kimapenzi baina ya Anna Makula na Mkola Vedastus wote wakiwa ni wakazi wa mtaa mmoja na wakiwa wamepanga nyumba moja huku wakiishi kama familia moja.
"Hawa wamepanga nyumba moja,huyu afisa hajaoa,kila mtu ana chumba chake inavyoonekana shemeji aliona wivu baada ya kuona kuna mwanamke ndani ya chumba cha shemeji yake ambaye ana mahusiano ya kimapenzi,hii ni hatari sana huyu jamaa alikuwa anafanya mapenzi na mke wa kaka yake",wameeleza mashuhuda hao.
Kwa upande wake mmiliki wa kituo cha Igalilimi Dk.Shija Luis amesema hali ya mgonjwa ni mbaya hasa kutokana na Afisa huyo kuunguzwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwa ni pamoja na sehemu za siri hivyo itachukua muda mrefu kumfanyia uchunguzi wa kina kwani ajali ya moto ni mbaya sana.
“Mara nyingi moto unasababisha maji kupungua sana maana joto kali la moto bado linaendelea kufukuta ndani kwa ndani ili kumnusuru ni kumwongezea dripu nyingi za maji na hivyo inatuwia vigumu kutoa taarifa za kidaktari mapema,majibu yatapatikana ndani ya siku tatu na kama ataendelea vibaya tutamhamishia hospitali ya Wilaya”,amesema Dk.Luis.
Naye kaimu mganga mkuu wa hospitali ya mji wa Kahama Deo Nyaga alipoulizwa kuhusiana tukio hilo amesema hana taarifa zozote zinazomhusu afisa wake.
Hata hivyo kaka wa Vedastus akijibu maswali ya wanahabari waliofika katika kituo hicho alikiri kutokea kwa hali hiyo katika familia yake ana kusema wamepanga nyumba moja na mdogo wake na wanaishi kama familia moja na kinachoendelea kati ya mkewe pamoja na mdogo wake katika tukio hilo alipigiwa simu na majirani na hajui chochote kuhusu kilichotokea.

Note: Only a member of this blog may post a comment.