Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mpinga alisema kikao hicho kilimalizika jana na kupitia malalamiko mbalimbali, hasa linalohusu sheria No.31 ya mwaka 2015, inayowataka madereva wa mabasi na malori kwenda kusoma, kuangalia afya zao na kujaribiwa kila baada ya miaka mitatu na kurudia kusoma (The Road Trafific Examination and Re-Testing of Drivers).
“Mchakato wa kanuni ya kuwataka kurudi kusoma ni utaratibu ulioanzishwa mwanzoni mwa Mwaka 2014, ukipitia katika hatua mbalimbali na kushirikisha wadau kutoka TRA, SUMATRA, NIT pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na vyama vya madereva nchini.
“Hitaji la kupata mafunzo ya muda mfupi (refresher course) kila baada ya miaka 3 lililoko kwenye kanuni zilizopangwa, linawahusu madereva wenye leseni za madaraja ya E, C, C1, C2 na C3 ambapo mafunzo hayo wanaweza kuyapata muda wowote kabla leseni zao hazijafika muda wa kuhuishwa na yeyote anayehitaji kupata leseni ya daraja E anaruhusiwa kupata mafunzo hayo,” alisema Kamanda Mpinga, katika mkutano uliofanyika Idara ya Habari, Maelezo.
Aidha, Kamanda Mpinga alisema hakuna sheria yoyote inayowataka madereva kurudi kusoma kwa mwaka wa huu au mwakani, lakini miaka ijayo sheria itakapokuwa tayari imekamilika, basi watalazimika kwenda kusoma maana pia itawawezesha kupata ujuzi zaidi kuliko walionao.
Mpinga alihitimisha kwa kusema madereva wote wa vyombo vya moto hawatakuwa na mafunzo wala kutakiwa kusoma mwaka huu, kwa kile alichosema mahitaji ya kanuni na mitaala ya mafunzo hayo hayajakamilika wala shule zitakazotoa mafunzo hayo hazijaainishwa, hivyo kukanusha uwepo wa ada ya shilingi 560,000/=.
PICHA/STORI:DENIS MTIMA/GPL

Note: Only a member of this blog may post a comment.