Wednesday, April 8, 2015

Anonymous

UTATA: MAPYA YAIBUKA POLISI ALIYEJIUA KITUONI TABORA

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda.
Tukio la kujiua kwa askari Polisi wa kituo cha polisi Sikonge, Tabora, PC Charles Mkoyi limechukua sura mpya baada ya ndugu kueleza utata wa majeraha aliyonayo ndugu yao na malalamiko yaliyoelezwa na marehemu siku chache kabla ya kukutwa na umauti. 

Ndugu wa marehemu huyo wamedai kabla ya kifo chake alilalamika kunyanyaswa na mmoja wa viongozi wa kituo hicho tangu alipoingia kazini.

Baadhi ya malalamiko aliyotueleza ni kupangwa zamu zisizo na mpangilio, kwa mfano, anakesha kazini badala ya kupumzika anatakiwa kurudi tena kazini…muda mwingi alikuwa anachoka sana na hata alipolalamika hakuwahi kusikilizwa na kiongozi huyo.” 

Alisema utata unaanza Kituo cha Polisi alichodaiwa alijipiga risasi kwa kuwa alitolewa haraka na kupelekwa Hospitali ya Mkoa, huku picha zilizopigwa kwa ajili ya kuonyeshwa familia na upelelezi, zikionyesha amekaa kwenye kiti akiwa amekumbatia silaha.

Tunavyofahamu eneo lolote lenye tukio la mauaji kama hayo, mtu haruhusiwi kufika wala kusafishwa hadi zipigwe picha na hata ndugu waone, lakini inaonekana walimnyanyua na kumkalisha kwenye kiti na kumpiga picha, kwa muda mfupi palisafishwa na mwili ukapelekwa Hospitali ya Mkoa. Tunajiuliza haraka hiyo ya nini?” alihoji ndugu huyo. 

Alisema kinachozua utata zaidi ni jinsi Charles alivyojipiga risasi kwa kuwa inaonyesha risasi iliingilia nyuma na kutokea mbele ambako kulikuwa na mfumuko mkubwa na nyuma tundu dogo, jambo ambalo lina shaka kwa kuwa kwa uelewa wa kawaida anawezaje kujipiga risasi kisogoni. 

Ndugu hao walidai baada ya kufika kwenye kituo hicho, walionyeshwa barua mbili zilizoandikwa na askari huyo, moja ikiwa ya kikazi na nyingine ya familia na kwamba walisomewa kiasi ya familia na ya kikazi haikusomwa na hawakupewa.

Tunajua mwili wa askari unaposafirishwa wanabeba na vitu vyake vyote, wanajua alikuwa hajaoa, hana ndugu, wameacha vitu vyake vyote, kesho tunavunja matanga ndiyo siku ya kugawana nguo za marehemu, kwa mazingira haya tutagawana nini?” alihoji ndugu huyo. 

Waliongeza kuwa hakukuwa na ukaribu wa polisi katika mazishi, alikuwa askari mwenzao lakini alizikwa kama raia wa kawaida.

Alisema walionana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda na kumueleza malalamiko yote na kuahidi kuyafanyia kazi, huku akisema ndani ya Jeshi la Polisi kuna utaratibu wa kufikisha malalamiko yoyote yanayohusu askari wao.
Waambie hao ndugu waje kuniona badala ya kulalamika kwenye vyombo vya habari,” alisema Kamanda Kaganda.
-NIPASHE

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.