Monday, April 6, 2015

Anonymous

Pluijm Wa Yanga: Wazimbambwe NOMA!

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm.
Na Martha Mboma,Bulawayo
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amesema haikuwa kazi rahisi kufuzu kutokana na aina ya mchezo na jinsi wapinzani wao, FC Platinum walivyokuwa wamejipanga katika mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika.


Licha ya timu yake kupoteza nafasi nyingi na kushindwa kuzifumania nyavu, bado Yanga imefanikiwa kusonga mbele kutokana na kuvuna mabao mengi katika mchezo wa awali ulipoigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, ingawa katika mchezo wa juzi iliambulia kipigo cha bao 1-0. 

Kocha huyo raia wa Uholanzi mwenye rekodi ya kuifunga Al Ahly ya Misri akiwa na Yanga, ameliambia Championi Jumatatu kuwa timu yake ilitakiwa kuibuka na ushindi, lakini umakini mdogo ndiyo uliowaponza na kutoka ‘kapa’ katika Uwanja wa Mandava mjini hapa. 

“Ukiangalia mchezo ulikuwa mgumu sana, wapinzani wetu walicheza tofauti na tulivyokuwa Dar. Walikamia na kutumia nguvu nyingi wakionekana kuna kitu walikuwa wakikitafuta.
“Lakini hata sisi tulikuwa na uwezo na kushinda mchezo huu, kwa sababu tulitengeneza nafasi nyingi lakini umakini mdogo ndiyo uliosababisha kushindwa kuweka mipira katika nyavu, hata hivyo, niwapongeze wachezaji wangu kwa sababu tumefanikiwa kusonga mbele,” alisema Pluijm akiwa na furaha. 

Yanga inarejea Tanzania kwa ajili ya Ligi Kuu Bara ambapo mchezo unaofuata inatarajiwa kucheza dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika Uwanja wa Taifa jijini Dar, keshokutwa Jumatano.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.