Niwapongeze kwa kuwa kapo ya mastaa ambayo kwa pamoja mnashirikiana kuhakikisha mnafanya vizuri kwenye muziki na maisha yenu yazidi kuimarika siku hadi siku.Madhumuni ya kuwaandikia barua hii ni kutaka kuwakumbusha kwamba mnatakiwa kuishi kama mastaa lakini msikiuke maadili yenu ambayo yanaweza kuwavunjia heshima katika jamii.
Nasema hivyo nikiwa na kumbukumbu nzuri ya matukio yenu ya chumbani ambayo mnayaonesha hadharani kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.Nimekuwa nikiyapima, mengi yanakuwa hayana sababu za msingi za nyinyi kuyaanika hadharani, achilia mbali sababu zenu binafsi.
Mwishoni mwa wiki iliyopita nilishuhudia moja ya picha yenu mliyopiga. Ilimuonesha Nuh ukiwa umetinga taulo huku umemshika makalio mpenzi wako Shilole aliyekuwa ameinama, tena mkiwa bafuni.Kwanza kabisa sikupenda picha hiyo maana haikuwa na mantiki. Mtajipigaje picha mkiwa bafuni? Mlikuwa na malengo gani? Mlitaka mashabiki wenu wajifunze nini kupitia picha hiyo? Majibu mnayo wenyewe.
Faragha huwa ni siri ya wapendanao, mnapokuwa chumbani, chooni na sehemu nyingine zinazofanana na hizo, zinahitajika busara kwani mazingira hayo yanakufanya wakati mwingine uwe umevua nguo.Sasa kwa nini uvue nguo halafu ujipige picha? Halafu mbaya zaidi, mwenzako kakushika katika eneo ambalo pia si zuri sana kila mtu kuona.
Kwa nini lakini mfikie hatua hiyo? Kama lengo ni kijipromoti katika kazi zenu, mbona zipo pozi nyingi ‘salama’ ambazo mnaweza mkapiga na mkafikisha ujumbe mlioukusudia?Angalia hata maoni ambayo watu waliyaandika baada ya nyinyi kuvujisha picha hiyo, kila mtu aliponda maana hakupata kitu cha kujifunza zaidi ya kuona mmefanya kitu cha kijinga ambacho kinavua heshima yenu.
Mbaya zaidi Shilole wewe sasa hivi ni mama wa watoto wawili. Watoto wako wanapaswa kuona unafanya mambo ambayo angalau yana staha kuliko kuona mambo ambayo mnayafanya mkiwa bafuni au chumbani.
Kabla ya kufanya mambo hayo, mnapaswa kujua kuna watu wengi ambao wataona mnachokitupia katika mitandao ya kijamii.
Kuna watoto kama wa kwako, kuna watu wazima ambao wamekuzidi umri pia wanatazama picha kama hizo.
Ili kulinda heshima yenu, ni vyema mkaachana na picha kama hizo badala yake mkaweka zile ambazo zinastahili kutazamwa na watu wote katika jamii.Kwa leo ni hayo tu, ni matumaini yangu mtabadilika. Niwatakie kazi njema.

Note: Only a member of this blog may post a comment.