Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana.
Wakati
serikali ikitangaza kuwarejesha Watanzania 21 kati ya 23 walioko kwenye
moja ya makambi yanayowahifadhi raia wa kigeni walioathirika na vurugu
zilizohusisha mauaji, uporaji na watu kukimbia makazi nchini Afrika
Kusini, Mtanzania aliyeko nchini humo, amesimulia jinsi raia wengi wa
kigeni walivyoathirika.
Joseph Moses, anayeishi mjini Durban, amesema pamoja na baadhi ya
raia wa kigeni kuawa, lakini waliothirika hadi sasa wengi wao hawajui
watalipwaje mali zao zilizopotea katika ghasia hizo.
Moses, ambaye alizungumza na NIPASHE kutoka nchini humo jana,
alisema kuna Watanzania wengi mjini Durban wamepoteza mali zao katika
vurugu hizo na hawajui watalipwaje.
Hata hivyo, alisema raia wa kigeni walioathirika zaidi na ghasia
hizo ni wanaotoka katika nchi za China, Pakistan, Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Nigeria na Somalia, baada ya maduka
pamoja na nyumba wanazoishi kuvamiwa na watu wanaosaidikiwa kuwa ni raia
wa Afrika Kusini na kuporwa.
“Kinacholeta utata ni kwamba, hata kama fidia itatolewa haijulikani
itakuwaje,” alisema Moses na kuongeza kuwa kuna idadi kubwa ya
Watanzania wanaoishi katika mji wa Durban ambao umeathiriwa zaidi na
vurugu hizo.
Alisema jana ulifanyika mkutano uliomhusisha Rais wa Afrika Kusini,
Jacob Zuma, Chifu wa Wazulu, Goodwill Zweluthini anayetuhumiwa
kuchochea vurugu hizo na viongozi wengine nchini humo katika kambi ya
waathirika hao mjini Durban.
Moses alisema katika mkutano huo, Chifu Zweluthini aliwapiga
marufuku raia wa Afrika Kusini kuendelea kuwashambulia raia wa kigeni.
Alisema sababu iliyotolewa na Chifu Zweluthini ni kwamba, nchi
nyingi za Afrika, ikiwamo Tanzania, ziliwasaidia weusi wa nchi hiyo
kuondoa siasa ya ubaguzi wa rangi.
Hata hivyo, alisema hakuna Mtanzania aliyeuawa katika vurugu hizo zilizosababisha mauaji ya raia wanane wa kigeni.
WATANZANIA 21 KUREJESHWA NCHINI
Wakati Moses akisema hayo, Watanzania 21 kati ya 23 walioko kwenye
kambi hiyo wamekubali kurejea nchini baada ya serikali kuwahakikishia
kuwalipia gharama za safari, lakini wawili wamekataa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa,
Watanzania wanaoishi Afrika Kusini wanakisiwa kuwa zaidi ya 10,000.
Alisema kati yao, 23 ndio waliobainika kuhifadhiwa katika kambi hiyo kufuatia kuibuka kwa ghasia hizo nchini humo.
Kutokana na hali hiyo, alisema serikali imekubali kugharimia safari
ya Watanzania hao 21 baada ya wenyewe kukubali kurejea nchini.
Alisema Watanzania hao 21 ni miongoni mwa raia wa kigeni ambao
baadhi wanasadikiwa kupoteza kazi na wengine shughuli zao za biashara
kuharibiwa katika ghasia hizo.
Ghasia hizo ziliibuka wiki iliyopita mjini Durban na kuenea katika miji mingine ya Johannesburg na Alexandria, nchini humo.
Alisema maofisa wa Tanzania kwa kushirikiana na ubalozi nchini
Afrika Kusini wanafanya uchunguzi ili kubaini Watanzania hao kila mmoja
alichopoteza, ikiwamo kazi na biashara katika ghasia hizo.
Waziri Membe alisema iwapo itabainika kuna walichopoteza, serikali za nchi hizo zitaangalia nini la kufanya kuwasaidia.
Alisema hadi sasa vurugu hizo zilizoibuka baada ya mmoja wa walinzi
ambaye ni raia wa kigeni katika duka moja kubwa Afrika Kusini kumuua
kwa risasi raia wa nchi hiyo wiki iliyopita, zimesababisha takriban raia
nane wa kigeni wanaotoka katika nchi za Ethiopia, Zimbabwe, Malawi na
Swaziland.
Hata hivyo, Membe alisema hakuna Mtanzania anayeishi nchini humo
aliyeuawa katika vurugu hizo na kwamba watu watatu wanaotuhumiwa
kuhusika na mauaji ya raia wa Msumbiji wamekamatwa katika msako mkali
unaoendelea nchini Afrika Kusini.
“Nimezungumza na Waziri wa Usalama wa Afrika Kusini, balozi,
wenzetu wa Zimbabwe, Mwenyekiti wa Sadc (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika), tumepeleka wenzetu wa Durban, swali kubwa je, tumepoteza
Watanzania wangapi? Hatujapoteza Mtanzania hata mmoja katika mgogoro
huo,” alisema Waziri Membe.
Aliongeza: “Nimekutana na Balozi wa Afrika Kusini leo (jana)
kumueleza masikitiko ya Tanzania na kumtaka kuhakikisha Watanzania
walioko Afrika Kusini wanakuwa salama.”
Hata hivyo, alisema kuna Watanzania watatu waliokufa katika matukio mengine matatu tofauti, ambayo hayahusiani na vurugu hizo.
Aliwataja Watanzania hao kuwa ni Athuman Mapepe, aliyekufa baada ya
kuchomwa kisu na wafungwa wenzake gerezani, Rashid Jumanne, aliyeuawa
kilomita 90 kutoka mjini Durban akiwa kwenye kitendo cha unyang’anyi na
Ally Heshima aliyefia hospitali jijini Johannesburg kwa maradhi ya kifua
kikuu na kwamba mwili wake ulirejeshwa nchini juzi.
Alisema Tanzania inaungana na Umoja wa Afrika (AU) kupitia
mwenyekiti wake, ambaye ni Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, pamoja na
Sadc kulaani vitendo vyote viovu walivyofanyiwa raia wa kigeni nchini
Afrika Kusini katika vurugu hizo, kwani ni kinyume cha haki za
binadamu.
KAULI YA CUF
Katika hatua nyingine, Chama cha Wananchi (CUF) kimesema
kinasikitishwa na machafuko yanayoendelea nchini Afrika Kusini dhidi ya
wakazi wasio wenyeji wa nchi hiyo, wakiwamo Watanzania.
“Haingii akilini hata kidogo baada ya muda mrefu kupambana na
makaburu kusaka uhuru wa Afrika leo hii waafrika tunaanza kufukuzana
wenyewe,” alisema Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Abdallah
Mtolea.
Aliongeza: “Ni wakati, ambao Waafrika Kusini wanapaswa kujua kuwa
si wao wanaopoteza ajira tu kwa kuwapo wageni nchini kwao, bali hata
mataifa mengine kama Tanzania pia ajira za raia wake zinapotea kwa
kuwapo wageni kutoka Afrika Kusini lakini tunavumiliana na hivyo ndivyo
tunapaswa kuishi.”
Aliitaka serikali ya Afrika Kusini kuongeza nguvu na kuharakisha
kukomesha vitendo vya kibaguzi, hasa kwa wageni wanaotoka nje ya nchi
hiyo.
Alisema kwa mujibu wa vyombo vya habari, Chifu Zweluthini amekuwa
miongoni mwa wachochezi wa kushambuliwa na kufukuzwa wageni nchini
humo.
“Ni wajibu wa serikali ya Afrika Kusini kumwajibisha kisheria ili matendo haya yasiendelee.
Tukizuia isitokee Afrika Kusini tutakuwa tumesaidia hali kama hii isitokee nchi nyingine za Afrika,” alisema Mtolea.
Alisema CUF ina taarifa kuwa Watanzania walioko Afrika Kusini ni miongoni mwa waliojeruhiwa na kufanyiwa vurugu.
“Kuna fununu ya Watanzania wawili kufariki dunia. Tunaitaka
serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake nchini Afrika
Kusini kuthibitisha hili ili kuondoa wasiwasi,” alisema Mtolea.
Aliongeza: “CUF tunajua ni wajibu wa kila Mtanzania kumlinda
Mtanzania mwenzake. Na ni wajibu wa serikali kulinda raia wake popote
pale walipo duniani. Serikali ya Tanzania haionyeshi kama
inawashughulikia Watanznaia walioko Afrika Kusini. Tunaitaka serikali
kubeba jukumu la kuwarudisha nyumbani mara moja Watanzania walioko
hatarini nchini Afrika Kusini.”
SOURCE:
NIPASHE

Note: Only a member of this blog may post a comment.