JAMBO LEO
Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe
amewataka wakazi wa Kigoma kutosikitishwa na mambo yanayomkabili kwa
sasa ila wamuunge mkono kwa hatua yoyote atakayoichukua kwa kuwa ni
wanasisasa wengi wamepitia katika misukosuko kama yake.
Zitto ametoa kauli hiyo Kigoma alipokutana na viongozi 250 wa vijiji Kigoma alipokutana nao jana.
“Msinililie
mimi kwa kuwa haya ni mapito ya kila mwanasiasa makini, wengi
walitofautiana na vyama vyao kwa sababu ya ya maslahi ya mataifa yao..
hivyo jukumu kubwa ni kuniunga mkono…”– Zitto Kabwe.
Mbunge huyo amesema hadi sana hajapewa
taarifa yoyote ya kusitishwa kwa Ubunge wake, lolote likitokea atarudi
kuwafahamisha juu ya uamuzi wake.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeanza kuchunguza malalamiko ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Wilbroad Slaa ya kutaka kulishwa sumu na Mlinzi wake.
Madai hayo ambayo yamekuwa gumzo katika
vyombo vya habari wiki hii huku wananchi wakihoji uhalisia wake,
yamemuhusisha mlinzi huyo wa Dk Slaa huku yeye mwenyewe akikataa tuhuma hizo na kudai kuwa ameteswa na walinzi wa CHADEMA.
Mlinzi wa Dk. Slaa
alidai kuwa ana majeraha mwilini yaliyotokana na mateso aliyofanyiwa
akiwa chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa usalama wa CHADEMA.
Kamanda Kova amesema kuna mambo mawili yanafanyiwa uchunguzi likiwemo la mlinzi Khalid Kagenzi
na la pili ni dhidi ya watuhumiwa wanaodaiwa kumtesa kwa kumshambulia
mlinzi huyo na kumsababishia majeraha mwilini mwake ambao ni Boniface Jacob ambae ni diwani kata ya Ubungo, Hemed Ally Sabula ambae ni Afisa Usalama wa CHADEMA na Benson Mramba mkazi wa Tabata Kisukuru ambaye ni Afisa Utawala wa CHADEMA.
Kova amesema shauri la kesi hiyo
litafikishwa mahakamani kupitia kwa wakili wa serikali ili
kujiridhisha kisheria na kutoa maamuzi kuhusu mashtaka yao.
TANZANIA DAIMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu
imenusa harufu ya ufisadi kwenye kivuko cha Mv Dar es Salaam ambacho
kinatarajiwa kuanza safari kutoka Dar kwenda Bagamoyo kupitia Kawe na
Mbezi Beach ambapo Kamati hiyo imebaini kuwa kivuko hicho ni chakavu na
cha zamani.
Kamati hiyo imebaini hayo wakati wa ziara ya kukikagua ambayo ilifanywa wakiwa wameongozana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Greyson Lwenje huku Mbunge Haroub Shamsi akisema kwamba thamani ya pesa zilizotajwa na uhalisia wake ni tofauti hivyo waliohusika kwenye manunuzi hayo wachunguzwe.
“Waheshimiwa
Wabunge siwezi kutoa maelezo ya kina hapa maana kuna waandishi wa
Habari, tusubiri kufanya kikao chetu wenyewe, nitaeleza kila kitu lakini
si hapa…” alijibu Naibu Waziri Lwenje na kufanya Wabunge hao kukasirishwa na kususia kumsikiliza Waziri huyo.
TANZANIA DAIMA
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya
Sekondari ya Wasichana Mpanda, Katavi wamekutwa wakiwa wamepoteza fahamu
kwenye bweni lao la na miili yao ikiwa imechanjwa chale bila wao
kujitambua.
Mkuu wa Shule hiyo Paza Mwamlima
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia jana shuleni hapo
ambapo bweni hilo lilikuwa na jumla ya wanafunzi 40 waliokuwa wamelala.
Siku ya jana asubuhi mwanafunzi mmoja
aliwahi kuamka ili awahi namba shuleni akawaacha wenzake wamelala,
Walimu walipoona wanafunzi wa bweni hilo hawaonekani walienda na kukuta
mlango umefungwa, baada ya kuufungua kwa nguvu walikuta wanafunzi hao
wakiwa katika hali hiyo.
MWANANCHI
Hali ya amani katikati ya Jiji la Mwanza
jana ilichafuka kutokana Polisi kupambana na wananchi, waliokuwa
wakipinga hatua ya madhehebu ya Kihindi ya Swaminarayan kujenga nguzo
makutano ya Mtaa wa Lumumba na Makoroboi ili kuzuia watu kukatisha eneo
hilo.
Eneo hilo lilikuwa lilikuwa likitumiwa na wamachinga, lakini viongozi wa hekalu hilo walimuomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo
kuwaondoa kwa sababu walikuwa wakiwabughudhi wakati wa ibada zao ambapo
Wamachinga 169 waliondolewa na kupewa eneo la Tanganyika ambako
wanaendesha biashara zao na sehemu hiyo kutumiwa na wapiti njia.
Jana wananchi walivamia eneo hilo na
kuanza kung’oa nguzo hizo, hali iliyosababisha kuitwa polisi ambao
walianza kutupa mabomu ya machozi.
Vurugu hizo zilidumu hadi saa 5:30
asubuhi na kusababisha maeneo ya Msikiti wa Ijumaa, Kituo cha Daladala,
Mtaa wa Lumumba na Barabara ya Nyerere yakitawaliwa na moshi wa mabomu
ya machozi.
Mtu mmoja amesema eneo hilo ni njia ya
umma ambayo inatumiwa na wananchi wengi, hivyo kitendo cha kuweka geti
kingezuia matumizi ya njia hiyo ya muda mrefu.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema wanawashikilia vijana 12 waliokuwa wanafanya fujo.
“Tulichofanya tumedhibiti wafanya fujo na sasa tunachunguza iwapo ujenzi huo ulikuwa na kibali,” alisema Kamanda Mlowola.
MWANANCHI
Wanafunzi watano wa Chuo Kikuu UDSM ni miongoni mwa watu walifariki katika ajali ya basi la Majinjah
iliyotokea Mafinga siku ya Jumatano baada ya kugongana na lori, huku
mwanafunzi mmoja akinusurika na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa Mbeya
ambako anapatiwa matibabu mpaka sasa.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Rwekaza Mukandala aliwataja wanafunzi hao waliofariki ambao ni Eric Killeo (mwaka wa tatu), Daud Sosten (mwaka wa tatu), Jeremia Watson (mwaka wa pili), Frank Mbaule (mwaka wa pili) na Didimo Chiwango (mwaka wa pili).
“Uongozi wa Chuo unatoa pole kwa wanafamilia wote pamoja na Jumuiya ya Chuo Kikuu. Tunamtakia mwanafunzi mwingine Rafael Nobert apate nafuu baada ya kujeruhiwa katika ajali hiyo”—Prof. Mukandala.
Wakati huo huo watu kutoka Malawi
wamefika nchini kwa lengo la kutambua miili ya ndugu zao kama nao ni
miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo huku mpaka sasa kukiwa
kumebaki miili ya watu wawili kutambuliwa kati ya watu 50 waliofariki.
-millardayo


Note: Only a member of this blog may post a comment.