Rais wa Simba, Evans Aveva.
Sweetbert Lukonge na Nicodemus Jonas, Dar es SalaamHATOKI mtu Taifa! Ndiyo kauli pekee unayoweza kutumia, baada ya uongozi wa Simba kuamua kuongeza nguvu ya watu watatu katika kamati ya mashindano, maalum kwa ajili ya kuiangamiza Yanga, wakati timu hizo zitakapovaana Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Taifa.
Kauli hiyo imetolewa na rais wa klabu hiyo, Evans Aveva katika mkutano mkuu wa timu hiyo uliofanyika jana Jumapili kwenye Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar.Miongoni mwa wanachama walioomba kamati hiyo kuimarishwa kuelekea mchezo huo, ni mdhamini mkuu wa timu hiyo, Ramesh Patel.
Wakati huohuo, Rais Aveva alifunguka sababu kadhaa zinazoifanya timu yao kuwa na mwendo wa kinyonga.“Ni kweli mwenendo wa kikosi chetu siyo mzuri, lakini mtambue kuwa kikosi chetu kina vijana wadogo ambao hawana uzoefu hivyo ni lazima tuwape muda wachezaji na kocha mwenyewe.
“Lakini pia hali ya timu kwa sasa kiuchumi haiko sawa, timu haina vyanzo vya kutosha vya fedha kulinganisha na matumizi yanayohitajika, kwani vyanzo tulivyonavyo vina uwezo wa kutuingizia milioni 30 wakati mahitaji ikiwemo kulipa mishahara wachezaji na wafanyakazi inatugharimu zaidi ya milioni 49 kila mwezi,” alisema Aveva na kufunguka kuhusu tetesi zilizozagaa kuwa haelewani na Geofrey Nyange ‘Kaburu’ pamoja na Simba Ukawa.
“Tangu tulipowaondoa wale wanachama 71 (kwa kosa la kufungua kesi mahakama za kiraia), mengi yameongelewa kuwa kuna mgogoro ndani ya uongozi, ndiyo maana timu inafanya vibaya, binafsi siamini katika hilo. Na kama wanataka yaishe, basi wafuate taratibu ikiwa ni pamoja na kuondoa kesi mahakamani. Kuhusu Kaburu, siyo kweli, mimi na yeye tunaelewana na tunashirikiana tangu enzi na enzi.” Licha ya kauli hiyo, minong’ono ya wanachama haikuisha, walisikika wakisema kuwa kuna migogoro ya ndani kwa ndani kwenye kamati na ndicho chanzo cha matatizo yote


Note: Only a member of this blog may post a comment.