Saturday, March 21, 2015

Anonymous

ACHA USHAMBA! FAHAMU NI VYA KIPUUZI KWELI LAKINI VINA MAANA KUBWA KWENYE MAPENZI!

NI Jumamosi nyingine mpenzi msomaji wa Love Story tunakutana katika uwanja wetu wa kuzungumza masuala mbalimbali yahusuyo maisha ya uhusiano.Niwashukuru wote ambao mnaendelea kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kuonesha mnanufaika na kile ambacho tunakijadili hapa kila Jumamosi.

Mada ya leo hapo juu inajieleza. Kwenye maisha ya uhusiano wengi wetu tunafanya makosa kwa wapenzi wetu pasipo kujua kama tunawakosea.Binadamu tulivyoumbwa ni dhahiri kwamba mara nyingi huwa tunajijali wenyewe kwanza kisha ndipo tunapowajali wenzetu. Inafika wakati tunajisahau kabisa kuwajali wapenzi wetu. Unapojijali wewe zaidi mkiwa tayari kwenye uhusiano, lazima anayetendewa atalalamika. 

Tatizo likiendelea hivyo licha ya mmoja wenu kulalamika matokeo yake ni ugomvi na hata kufikia hatua ya kuachana. Ili maana ya mapenzi ikamilike, mnapoanzisha uhusiano wa aina yoyote lazima dhana ya ‘umimi’ iondoke ndipo muweze kudumisha penzi lenu. 

Mwanamke anapaswa kumjali mwanaume kwa kiasi ambacho yeye anajijali au ikiwezekana hata zaidi. Vivyo hivyo kwa mwanaume, anapaswa kumjali mwanamke katika hatua ambayo yeye anajijali au ikiwezekana avuke ili kuongeza utamu zaidi wa mapenzi.
Kumjali mtu si lazima umpe fedha au vitu vya thamani kubwa. Kuna vitu vingi sana ambavyo unaweza kuvifanya na mwenzi wako akaona unamjali. Unaweza kuona ni vya kipuuzi lakini usipomfanyia vinaweza kuwa shubiri katika penzi lenu. 

Hapo ndipo kwenye msingi wa hoja yangu ya leo. Ukiachana na vitu vikubwa vya thamani kama vile kumjengea nyumba, kumnunulia gari, kumpangia ofisi na mambo mengine yanayofanana na hayo, kuna vitu ambavyo kwa macho ya kawaida vinaonekana ni vidogo lakini katika mapenzi vina maana kubwa. 

Nasema vina maana kubwa sababu mapenzi siyo fedha, mapenzi ni utu na kujaliana. Wewe umjali mwenzako na yeye akujali. Mapenzi yanataka hali ya ‘nipe nikupe’ ili wote mpate raha. Hamtakiwi kunyimana, hamtakiwi kufichana, mnatakiwa kuaminiana.
Vifuatavyo ni vitu vidogovidogo ambavyo wengi wetu tunaviona ni vya kipuuzi kutokana na ubize wa kazi au kwa makusudi, tunaamua kuviacha pasipokujua vina maana kubwa sana katika mapenzi:

ZAWADI NDOGONDOGO
Suala hili wengi wetu tunajisahau kulifanya. Watu wanaona kwamba zawadi ni kumnunulia mpenzi wake kitu kikubwa, hapana. Kuna zawadi ndogondogo ambazo unaweza kumnunulia kwa kuona ni kitu kidogo lakini kwake kikawa ni kitu kikubwa sana. 
Mfano unajua kabisa mpenzi wako anapenda Ice Cream, unapokuwa unarudi nyumbani au unakwenda kumtembelea, ukimnunulia atajisikia furaha sana. Atafurahi kwa sababu kwanza ni kitu anachokipenda lakini pia furaha yake inazidi kuongezeka sababu anaona unamjali kwa kumkumbuka na kumnunulia kitu hicho anachokipenda. 

Ice Cream ni kitu kidogo, thamani yake ni ndogo lakini kina maana kubwa sana. Huo ni mfano wa zawadi ndogo, hiyo inategemea na maeneo uliyopo. Jenga utamaduni wa kumpa mwenzi wako zawadi ndogondogo, zinasaidia sana kudumisha penzi lenu. 

KUMPIGIA SIMU/SMS
Huu ni ulimwengu wa mawasiliano ya simu. Asilimia kubwa ya wapendanao wana simu. Suala la wewe kumpigia simu mpenzi wako ni la msingi sana. Mpigie hata kama huna hata kitu cha msingi cha kumueleza lakini unaweza kujali hata nyakati. Kujua kwamba huu ni wakati wa chakula labda cha mchana, si vibaya ukimuuliza umekula? Hata kama huna uwezo wa kumpa hicho chakula lakini unapomuuliza, anatambua upendo wako. 

Kama unatambua kwamba mwenzako yupo bize , mtumie hata ujumbe mfupi wa maneno wa kumtaka akumbuke kula. Muulize umeshindaje kama ni jioni, mueleze kwamba umemkumbuka. Inasaidia sana, hiyo pia inapendeza mkiifanya wote wawili. Mwenzako akikufanyia kitu kama hicho na wewe mfanyie, inasaidia sana.
Itaendelea wiki ijayo.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.