Tuesday, March 8, 2016

Anonymous

Mwalimu Auawa Kwa Risasi Jijini Dar! Mkasa Kamili Nimekuwekea Hapa

mwalimu (1) 
Mwalimu Grace Benedicto, enzi za uhai wake.
Stori: Makongoro Oging’na Issa Mnally, UWAZI
DAR ES SALAAM: Mwalimu wa Shule ya Msingi Msigani, Kimara wilayani Kinondoni jijini Dar, Grace Benedicto 32, (pichani) ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakati alipokuwa akijiandaa kwenda kumpokea mume wake kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kuwa, mauaji hayo yalitokea saa mbili usiku wa Februari 27, mwaka huu huko Msigani, Mbezi, Dar hatua chache kutoka shule aliyokuwa akifundishia mwalimu huyo. mwalimu (2)
Kwa mujibu wa majirani wa eneo hilo, siku hiyo watu watatu walifika kwenye duka la huduma ya pesa na vocha la mwalimu huyo wakiwa kwenye pikipiki moja, mmoja wao alitoa shilingi elfu kumi ali apewe vocha, mwingine alihitaji Luku.
“Lakini ghafla wakamuweka mwalimu chini ya ulinzi. Hata hivyo, alipambana nao, wakamzidi nguvu na ndipo mwingine aliyejificha mahali akatoa bunduki na kumfyatulia risasi mbili mwalimu.

“Risasi moja ilimpiga bega la kushoto, nyingine tumboni. Alidondoka chini huku akipiga kelele ya kuomba msaada lakini tulipofika tulikuta wale majambazi wameshakimbia,” alisema jirani mmoja.
Aliendelea kusema kuwa, polisi walitaarifiwa na walifika katika eneo la tukio muda mfupi na kumchukua mwalimu kumkimbiza Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Kibaha mkoani Pwani lakini daktari alipomchunguza akagundua alishafariki dunia.
Uwazi lilifika msibani, Kimara ya Stop Over jijini Dar na kuzungumza na mdogo wa marehemu aitwaye Benard Benedicto ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Ninachojua mimi siku hiyo dada alikuwa akifunga duka ili akampokee shemeji uwanja wa ndege lakini muda mfupi kabla ya kuondoka, ndipo walifika hao majambazi.
“Dada alikuwa akiwasiliana na mume wake hadi pale mume wake alipozima simu baada ya kupanda ndege. Aliposhuka na kuwasha simu ili ampigie dada, akapokea taarifa ya mkewe kupigwa risasi, lakini muda huohuo akapigiwa simu kuwa, amefariki dunia.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Dustan Kuzirwa katika mahojiano na Uwazi ofisini kwake wiki iliyopita alisema kuwa, wamesikitishwa na mauaji hayo ya kinyama ya mwalimu Grace.

“Mwalimu Grace alikuwa mchapa kiazi na mwenye ushirikiano mkubwa na wenzake. Alikuwa kitengo cha kompyuta na alianza kazi mwaka 2006. Tunalaani mauaji hayo na tunaliomba jeshi la polisi kuwasaka wahusika,” alisema Dustan.

Hata hivyo, mume wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Kimati alipohojiwa alisema waliomuua mkewe siyo majambazi bali kuna siri nyuma yake. Hakuitaja.
Mazishi ya mwalimu huyo yalifanyika katika makaburi ya Banda la Mkaa, Mbezi Jumatano ya Machi 2, mwaka huu.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.