Stopa tegemeo wa Mtibwa Sugar, Salim Mbonde.
Nicodemus Jonas, Dar es Salaam STOPA tegemeo wa Mtibwa Sugar, Salim Mbonde, amefunguka kuwa yupo njiani kumalizana na Simba, ikiwa ni siku chache baada ya nyota huyo kutoroshwa kambini na kwenda kufanya majadiliano kuhusu dili la kumwaga wino kwa ajili ya msimu ujao.
Nyota huyo ambaye ni mchezaji bora wa Michuano ya Mapinduzi ya mwaka huu, alikoswakoswa na Simba katika usajili wa msimu huu, kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Mganda, Juuko Murshid, lakini tayari Simba imeanza tena mikakati ya kumnasa kwa ajili ya kuimarisha safu ya kati ya ulinzi inayoonekana kupwaya mpaka sasa.
Habari za kina zinasema kuwa, Mbonde alitoroka kambini hivi karibuni wakati timu yake ikiwa jijini Dar es Salaam ikijiandaa na mchezo na Azam, ambao Mtibwa ilifungwa mabao 5-2.
Habari zinaeleza kuwa Simba ilimtengea kitita cha milioni 20, lakini mchezaji mwenyewe alitaka kitita cha milioni 35, ambapo Hans Poppe alimtaka kuwa na subira ili suala lake lifikishwe kwenye kamati ya usajili na jibu atapewa muda wowote kwa kumwambia kuwa kama ni suala la hela kwao ni kitu kidogo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mbonde alifunguka: “Mimi ni mchezaji na hii ndiyo ajira yangu, hivyo naangalia wapi penye upepo mzuri, sitaki kuzungumzia kwa kina hilo suala, lakini ni kweli nilifanya mazungumzo na Simba lakini hatukuafikiana, ila iwapo watatimiza nilichowaambia, nitasaini, sina kinyongo nao.”
Alipotafutwa Hans Poppe alikanusha na kusema kuwa hawajafanya mazungumzo na mchezaji yeyote.
Mmoja wa viongozi wa juu wa Mtibwa Sugar, ameliambia Championi Jumatano kuwa, Mbonde alisaini mkataba wa miaka miwili ambayo inamalizika mwishoni mwa msimu huu, huku akienda mbali na kusema ni vigumu kumbakiza kutokana na msimamo wake kwa sasa wa kutaka kuondoka.
JIUNGE NASI FACEBOOK > >>BONYEZA HAPA.KAMA KUNA TATIZO AU
UNA PICHA ZA MATUKIO TUTUMIE WHATSAPP +255 712 919 142.
ASANTE NA KARIBU
TENA!


Note: Only a member of this blog may post a comment.