Tuesday, February 24, 2015

Anonymous

NINI PAUL MAKONDA? HATA WEWE UNAWEZA KUWA MKUU WA WILAYA

Paul Makonda.
PAUL Makonda mteule wa Rais Jakaya Kikwete kwa nafasi ya ukuu wa Wilaya ya Kinondoni, ameibuka kidedea wa wapingwaji wa nafasi hiyo. Wasomi na wachambuzi wa mambo wamekosoa uwezo wake kwa sababu mbalimbali lakini kubwa zaidi ni ‘utoto’wake unaounganishwa na tukio la vurugu alizofanyiwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Jaji Joseph Warioba. 

Uteuzi wa Makonda umekuwa gumzo kiasi cha watu kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhoji sifa za mtu kufaa kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya, (nafikiri wanahoji hivyo kwa sababu wanamuona kijana huyo hana vigezo),  jambo ambalo nimeliona ni la msingi zaidi kulijadili kuliko Makonda mwenyewe. 

Wakati nafuatilia mijadala ya anafaa au hafai nilishindwa kuelewa kutokana na hoja dhaifu za upande wa ukosoaji; maana wapo waliomkosoa kwa kusema, alimshambulia mzee Warioba hivyo hakustahili kupewa nafasi hiyo; hoja inayowafanya wanaopinga kupoteza mwelekeo kwa sababu hata Waziri wa Kilimo na Ushirika, Steven Wassira ‘Tyson’ aliwahi kumpiga mwandishi na leo ni waziri anayefanya vyema. 

Hoja nyingine iliyojengwa ni kwamba Makonda amepewa nafasi hiyo kama shukurani za unyenyekevu wake kwa rais na familia yake na wengine kufika mbali kwa kusema anapongezwa kwa kumshambulia Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa. Hayo nawaachia watoa hoja.
Binafsi najiuliza hivi; majukumu hasa ya mkuu wa wilaya ni yepi hata yampwaye Makonda na kuhitaji akili ya tatu kuyatimiza? Niliozungumza nao hawakunijibu kinagaubaga.Mfumo wetu wa utawala una majibu yote; lakini watu hawataki kuushambulia, badala yake wanawashambulia wateule kwa kuwahusisha mpaka na mambo binafsi. 

Miongoni mwa kazi za mkuu wa wilaya ni uwakilishi wa rais sehemu husika, uenyekiti wa kamati ya ulinzi ya wilaya, kupokea wageni na kuwatembeza kwenye eneo lake pamoja na kuwadhibiti wanaokwenda kinyume na matakwa ya serikali! Makonda atashindwa? 

Atashindwa kupokea Mwenge na kuhutubia wananchi kwenye mialiko ya kiserikali;  hiyo ni kazi ngumu inayohitaji akili za kiwango cha juu? Ndiyo maana nimesema; nini Makonda? Hata wewe ukipewa wilaya utaweza kwa sababu hakuna majukumu maalum na mazito ya kufanya kila siku. 

Kwa msingi huo, sifikirii kama kuna siku wanaomkosoa Makonda watakuwa na kitu cha kumhukumu kuwa hajakisimamia vizuri kwa sababu ukuu wa wilaya hauna  kipimo cha ufanisi. 

Mara kadhaa nimeandika kwamba kutokana na mfumo wa kiutawala nafasi ya mkuu wa wilaya haina maana; hawa ni watu ambao wanaingozea mzigo serikali bila sababu. Siyo jambo sahihi kwa mkuu wa wilaya asiyekuwa na kazi akanunuliwa gari, akawekewa mafuta, akalipwa mashahara na watumishi wake, halafu uzalishaji wake ukawa ni ziro. 

Wananchi lazima wahoji ni kwa nini kodi zao waendelee kulipwa mishahara watu ambao pengine rais na watendaji wake wanawashukuru kwa sababu wamewafanyia mambo binafsi?

Ningependa kuona makujumu ya kusimamia wilaya zetu yanabaki chini ya wakurugenzi ambao sheria za serikali za mitaa zimewapa uhuru wa kujiamulia mambo  bila kuingiliwa, hili litasaidia kuokoa fedha nyingi zinazopotea kwa kuwahudumia wakuu wa wilaya ambao si wazalishaji. Huku ndiko kubana matumizi tunakokulilia kila siku. Mungu asaidie tupambane na mfumo wetu mbovu na kamwe tusipambane na watu wanaoutumikia kama akina Makonda. Nachochea tu.
JIUNGE NASI FACEBOOK > >>BONYEZA HAPA.KAMA KUNA TATIZO AU UNA PICHA ZA MATUKIO TUTUMIE WHATSAPP +255 712 919 142. 
ASANTE NA KARIBU TENA!

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.