Monday, December 26, 2016

Unknown

"Nashangaa Watu Wanapolia Ugumu wa Maisha" - Askofu PENGO

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewashangaa watu wanaolalamika maisha ni magumu wakati serikali ya awamu ya tano imejitahidi kuboresha miundombinu yenye kuleta unafuu wa maisha.

Katika salamu zake za Krismasi kwa Watanzania, Askofu Pengo alisema hali ya maisha kwa sasa imeboreka zaidi kwani barabara nyingi zimetengenezwa kurahisishia usafirishaji wa biashara kati ya nchi na nchi jirani na kati ya mkoa na mkoa.

Pia alisema kitendo cha Serikali kununua ndege kadhaa kwa ajili ya Kampuni ya Ndege (ATCL) kumerahisisha maisha ya Mtanzania kwani kunawezesha watu kusafiri kwa haraka kwa gharama ndogo.
“Kwa mfano Arusha kwa ndege tulikuwa tunaenda kwa Sh 800,000, lakini sasa hivi unaweza kwenda kwa gharama kati ya Sh 360,000 na Sh 400,000 kwa kutumia ndege za Serikali, napata shida kusema hali ya maisha ni ngumu,” alisema Askofu Pengo.


Kuhusu amani Pengo alisema katika awamu hii ya tano, kuna amani kubwa na akatoa mfano wa kisiwani Zanzibar kuwa siku za nyuma watu waliishi kwa wasiwasi mkubwa kutokana na watu kumwagiwa tindikali na viongozi wa dini ya Kikristo kupigwa risasi, lakini sasa hivi kuna amani kuliko wakati uliopita.

“Kule Zanzibar, hali ilikuwa ya kutia mashaka, sisi hatukujua tukimbilie wapi kutokana na mashambulizi yale yaliyolenga watu wa dini moja, lakini kwa sasa amani ni kubwa zaidi kuliko awamu iliyopita,” alisema Askofu Mkuu Pengo.

Aliwakumbusha Watanzania kwamba kila mtu akisimama na kutambua wajibu wake wa kudai amani, hali itakuwa nzuri zaidi. Pia alitoa mwito Watanzania wasifarakane kwa sababu ya dini na akawataka waamini wa Kikatoliki wawe wa kwanza kutetea amani na mapatano dhidi ya watu wa dini nyingine.

Pia alisema pamoja na tofauti za dini na itikadi za kisiasa, Wakatoliki wanatakiwa kuwa na msimamo wa kutetea umoja na amani.
Asema amani italetwa na masikini, si matajiri

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.