STORI: DUSTAN SHEKIDELE, WIKIENDA
Morogoro: Haijawahi kutokea!
Kwenye Kijiji cha Melela, Mlandizi wilayani Mvomero mkoani hapa,
kumegubikwa na simanzi nzito kufuatia maiti ya mtoto, Rahim Fikiri (2),
kukumbwa na mauzauza kibao yakiwemo kupiga kelele wakati wa kuoshwa,
mwili kutoka jasho kali na kuliwa macho na masikio.
MASHEHE WALAZIMIKA
Tukio hilo la kusikitisha lilijiri wiki
iliyopita nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo kijijini Melela, Mlandizi
hivyo kuwalazimu mashehe kuingilia kati na kushusha dua nzito
iliyoondosha mauzauza hayo.
Kufuatia tukio hilo, baadhi ya wananchi
wa kijiji hicho walimtonya mwanahabari wetu aliyefika katika kijiji
hicho kilichopo umbali wa kilomita 40 kutoka mjini Morogoro ambapo
alikutana na msafara wa kuelekea makaburini kwa ajili ya mazishi.
Bibi wa marehemu, Elizabeth Josefu.
BIBI ALIYESHUHUDIA
Akizungumzia tukio hilo, bibi wa marehemu aliyeshuhudia mauzauza hayo, Elizabeth Josefu alikuwa na haya ya kusema:
“Nilipigiwa simu nikaelezwa kwamba
mjukuu wangu amelazwa Kituo cha Afya cha Melela. Nilipofika nilielezwa
kuwa alipopimwa, alikutwa ana upungufu wa damu.
“Aliongezewa
damu na baba yake lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya hivyo tulipewa
rufaa ya kumpeleka Hospitali ya Mkoa. Tulipofika huko tuliambiwa ana
degedege lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia wakati akipatiwa
matibabu.
“Tulichukua maiti, tukarejea nyumbani. Tulipofika na kuifunua tukaiona inatoka jasho kali hivyo tukaimwagia maji bakuli mbili.
“Wote tuliogopa tukakimbia, tuliporejea
ndani, akatokea paka mkubwa mwenye rangi nyeusi, tukakimbia tena, akaja
bibi mmoja hatumfahamu akamfukuza.”
Bibi
huyo alisema kuwa, baada ya kuona hali hiyo, yeye na wanawake wenzake
walibeba jukumu la kuiosha maiti hiyo ambapo wakati wanamnyoosha mkono
wa kulia, marehemu huyo alipiga kelele za mtoto anayelia akilalamika
maumivu, jambo lililoibua hofu kubwa hivyo watu wakakimbia.
“Tukio lingine ilikuwa usiku, tulipoifungua maiti tulikuta panya wamekula macho na masikio.
“Baada ya msururu wa mauzauza, wazazi wa
marehemu waliwaita mashehe waliosoma dua ndipo hali ikatulia na muda
huu tunakwenda kuzika,” alimalizia bibi huyo huku akiangua kilio.
Baba wa marehemu, Fikiri Mrisho
BABA WA MAREHEMU
Kwa upande wake baba wa marehemu, Fikiri Mrisho alipohojiwa na Wikienda alisema:
“Inaniuma sana kwani licha ya kumpoteza mwanangu bado anaendelea
kuteseka kwa mambo ya kishirikina. Hebu fikiria mwili wake kuliwa na
panya! Haya ni mambo ya kutisha.”
NENO LA MWENYEKITI
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Melela,
Yusuf Ally Nguwa alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alikiri kutokea na
kusema serikali haiamini mambo ya kishirikina.
Mtoto huyo alizikwa kijijini hapo huku
wengi wakidai mambo hayo ni kawaida kwa Waluguru japokuwa katika tukio
hilo hali hiyo ilipitiliza.
Note: Only a member of this blog may post a comment.