Monday, May 9, 2016

Anonymous

Mama wa SNURA Aanguka Ghafla... Ndugu Waja Juu... SNURA Anyooshewa Kidole!

Wakati Wabongo wakiwa wamecharuka mitandaoni kuuzungumzia wimbo wa Chura wa Snura Mushi, nyuma ya mijadala hiyo, kuna habari ya kuhuzunisha, mama mzazi wa msanii huyo, Doto Sanzegara, alijikuta akianguka kwa mshtuko baada ya serikali kutangaza kumzuia mwanaye huyo kujihusisha na kazi za sanaa, Ijumaa Wikienda linakupa zaidi.
ALIZUIWA NA BASATA
Serikali kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) walitoa tamko la wimbo huo kutopigwa katika vituo vya redio na televisheni nchini pamoja na kwenye mitandao ya kijamii kwa kile walichoeleza kuwa umekiuka maadili hivyo pia kumfungia kazi zake mpaka pale atakapojisajili katika chombo hicho kwa kuwa licha ya kufanya kazi za sanaa kwa muda mrefu, msanii huyo hakuwa amejisajili. 

HABARI KAMILI
Kwa mujibu wa chanzo kilicho karibu na familia, wakati serikali inatoa tamko la kumsimamisha Snura, Mei 4, mwaka huu, mama huyo alipata taarifa kupitia redio, ndipo alipopata mshtuko, akaanguka na kupoteza fahamu. “Yaani ile anasikia tu redio inatangaza, mama alikuwa amekaa kibarazani, akaanguka palepale ghafla. Ikawa mshikemshike kunusuru uhai wake. Ikabidi ndugu waliokuwa pale nyumbani waanze kumpa huduma ya kwanza kwa kumpepea.

APEPEWA
“Walianza kumpepea pale nyumbani huku wengine wakitafuta usafiri wa kumpeleka Mwananyamala Hospitali, lakini bahati nzuri kabla hawajapata gari, mama alizinduka na kurejea katika hali ya kawaida.

WAMPA UANGALIZI MZITO
“Ilibidi baadhi ya ndugu ambao walikuwa mbali wasogee nyumbani kwa ajili ya kumwangalia afya yake kwa ukaribu zaidi,” kilisema chanzo hicho.

MAMA ANA TATIZO HILO
Chanzo hicho kilizidi kuweka wazi kuwa, mama Snura huwa ana tatizo hilo hususan pale anapopata habari ya mshtuko na kwa sababu Snura alikuwa miongoni mwa watoto ambao amekuwa akiwategemea, habari za kufungiwa zilimshtua sana. “Bi mkubwa aliona ni janga maana Snura ndiyo kila kitu kwake. Anajitoa sana kumsaidia mama yake hivyo kitendo cha kufungiwa sanaa, kilimpa tafsiri ya haraka kuwa pengine watakufa njaa,” kilisema chanzo hicho. 

APEWA HABARI NJEMA
Baada ya kurudi katika hali yake ya kawaida, mama Snura alipewa taarifa kuwa mwanaye huyo ameshakamilisha taratibu zote zilizotakiwa na Basata hivyo yupo huru kuendelea na sanaa lakini kwa angalizo la kuufanya upya wimbo wa Chura kwa kutoa
sehemu ambazo zimekiuka maadili.
 
NDUGU WAMYOSHEA KIDOLE SNURA
Mjomba wa Snura ambaye hakupenda jina lake lichorwe gazetini alilieleza Ijumaa Wikienda kuwa kutokana na tukio hilo, wamemuonya msanii huyo kuwa makini na kazi zake za sanaa ili zisiweze kumsababishia matatizo mzazi wao. “Tumemuonya maana katika hili hana sababu ya kujitetea. Yeye ndiye sababu ya mama yake kuanguka. Tumemwambia awe makini maana asingetoa Chura ambayo imekiuka maadili wala hiyo serikali isingetamka kuwa inamfungia,” alisema mjomba huyo.

SNURA HUYU HAPA
Baada ya kuzinyaka habari hizo, Jumamosi iliyopita, mwanahabari wetu alimvutia waya Snura ambaye alikuwa safarini kuelekea jijini Mwanza ambapo alipopokea alikiri kumsababishia mshtuko huo mzazi wake, lakini akasema anamshukuru Mungu suala hilo limepita salama. “Wee ilikuwa mbaya sana lakini namshukuru Mungu limepita salama. Mama yuko poa, mimi naendelea na mizunguko ya kazi zangu za sanaa, Chura anakuja kivingine hivyo mashabiki wakae mkao wa kula,” alisema Snura.

KUMBUKUKUMBU
Kabla ya kutoa wimbo wa Chura, Snura ametoa nyimbo kadhaa zilizotamba mjini ikiwemo Majanga ambayo bado inaendelea kufanya vizuri katika anga la muziki.
CHANZO: IJUMAA WIKIENDA

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.