Rama D
Makala: Andrew Carlos
UKITAJIWA jina la Ramadhan Shaibu kisha ukaambiwa ni
mfalme wa Muziki wa R&B nchini ni wazi utakataa hakuna msanii kama
huyo, na ukiambiwa kuwa mara nyingi hutumia muda wake kuwa Brisbane,
Australia na familia yake bado utakataa.
Lakini ukitajiwa jina la Rama D bila kumalizia utadakia na kusema
kuwa unamjua na ni bonge la msanii wa R&B Bongo kuwahi kutokea, moja
kwa moja utaanza kumsifia kwa sauti yake ilivyotumika vyema kwenye
wimbo wa Nikki wa Pili uitwao Good Boy na baada ya hapo utataja listi
ndefu ya nyimbo zake zikiwemo Sio Waoaji, Kama Huwezi, Kikao cha Family,
Kuwa na Subira, Usihofie Wachaga, Make Up na wa sasa ambao ni Kipenda
Roho.
Rama D
Over Ze Weekend lilipata fursa ya kufanya makala
‘exclusive’ kutoka Brisbane, Australia ambapo yupo kwa sasa na familia
yake akiwa ameoa Mzungu na kufanikiwa kuwa na mtoto mmoja.
Katika makala haya anafunguka zaidi;
Safari ya muziki
“Muziki nilianza kama utani, nakumbuka zamani nilikuwa napenda sana
kusikiliza miziki ya aina yote, nikawa naimba kwenye sherehe za kuzaliwa
‘birthday’ za marafiki zangu huku nikitumia midundo ya Nate Dogg
(marehemu), Tyrese na wengine kibao.
“Baadaye nikahamia kwenye soka, lile eneo la Mlimani City kulikuwa na
uwanja wa mpira ambapo nilikuwa mchezaji wa Timu ya Survey. Sasa kila
siku nikirudi kutoka mpirani njia yangu kubwa ilikuwa ni lazima nikatize
nyumbani kwa kina Mr. Paul (mwimbaji wa zamani wa R&B) na
niki-katiza dirishani kwake nilikuwa nikimsikia akiimba ‘akapera’ kwa
sauti kubwa, nikajiuliza hivi anavyoimba huyu si hata mi naweza? Basi
nikajaribu kuingia studio ikawezekana lakini kuimba kwangu kukawa ni kwa
kujifurahisha tu.
Rama D akiwa na mkewe na mwanaye
Unazungumziaje Muziki wa R&B Bongo?
“Wasanii wengi wa R&B nchini kwa sasa wanafanya poa nawasikia ni
kitu cha kujipongeza hasa sisi Wabongo kuuelewa muziki huu kwani
mwanzoni wengi waliutenga na kubaki kuwa ni muziki wa watu wachache.
Kwa nini wana Bongo Fleva wengi hukimbilia kurekodi nje ya nchi?
“Ujue kila mfanyabiashara anakuwa na lengo lake. Mwingine anataka
kufanya video nje ya nchi ili mastaa waweze kumuona. Unakuta
mtayarishaji wa video wa Sauz ana mawasiliano mazuri na vituo vikubwa
vya TV kwa hiyo msanii wa Bongo anakimbilia hapo kwa kuamini
atajitangaza Afrika nzima.
“Ushauri wangu kwao, kwanza tusiwe na haraka za kukimbilia huko, pili
tuwakubali watayarishaji wetu na tuwape bajeti ambayo watakutengenezea
video unavyotaka iwe.
Staa gani unamkubali kimataifa?
“Nampenda sana mdada mmoja hivi wa Nigeria anaitwa Asa, yupo vizuri kuimba na mashairi.
“Pia nawapenda sana Sauti Sol na naamini kabisa ipo siku nitakuja
kufanya nao kolabo kwani wao ni waimbaji wazuri na wakikutana na
mwanamuziki mzuri kama mimi lazima kitu kitoke kizuri zaidi,” anamaliza
Rama D.
Note: Only a member of this blog may post a comment.