Wiki iliyopita tuliishia pale Mkwere
alipopata msiba na kuchukuliwa na kaka zake ambao walimlea
wakishirikiana na baba yake mdogo, Richard Rafael ambaye naye alikuja
kufariki dunia. Pia aligusia kwa ufupi ukoo wao ulivyochanganyika dini
mbili yaani Wakristo na Waislamu…
Songa naye…
Songa naye…
“Mwaka 1998 nilifanikiwa kuanza sekondari katika shule ya jeshi ya Makongo iliyopo Makongo jijini Dar, kama ilivyokuwa kwa shule ya msingi na hata sekondari somo la hisabati kwangu lilikuwa ni kama mzimu unaoniandama kwani lilikuwa ni gumu zaidi, ila somo la historia, jiografia, uraia, Kiswahili na Kiingereza ilikua ni rahisi kwangu.
“Nakumbuka pia wapo wanafunzi wengi niliosoma nao pale Makongo ambao kwa sasa wana maisha yao tofauti na wengine ni watu maarufu tu, miongoni mwao ni Jose Mara, MC Babu Ayoub na wengineo wengi, nakumbuka niliwahi kushindana na Jose Mara (ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa Bendi ya Mapacha Watatu) na katika mashindano yale nilimshinda vibaya.
“Naweza kusema hata kucheza muziki niko vizuri, kwani kutokana na umahiri wangu wa kukata nyonga kampuni ya vinywaji baridi ambayo miaka ya nyuma ilikuwa na maonesho yake kama unakumbuka, iliwahi kunipa mkataba wa kunisomesha miezi sita pamoja na mikataba mingine midogomidogo na hii ni baada ya kuibuka kidedea kwenye moja ya shoo zao.
“Wakati nikiwa nasoma sekondari nilikuwa msafi sana na nilikuwa napenda kwenda shule nikiwa nimepulizia pafyumu si unajua tena ujana mwingi, sasa kuna siku nilichelewa shuleni na kukuta wenzangu wakiwa mstarini.
“Siku hiyo kulikuwa na mwalimu mmoja alikuwa akiitwa Afande Miraji (kwa sasa ni marehemu), alinisogelea kwa karibu akahisi harufu ya ‘unyunyu’ (pafyumu) alichokifanya ni kunipa adhabu ya kumkumbatia beberu, dah! Msomaji si unajua beberu alivyo na harufu basi nguo na mwili wangu wote nikawa nanukia kimbuzimbuzi tu, kiukweli ilinikera sana hali ile.
“Afande Miraji kwangu alikuwa ni zaidi ya mwalimu na afande pia kwani adhabu mbalimbali alizokuwa akinipa nahisi zilinifanya kukomaa zaidi na kuwa imara katika maisha yangu ya sasa.
“Kingine ninachokikumbuka ni tabia yangu ya kulakula hovyo, basi siku hiyo nikiwa mstarini mwalimu aliniotea nikiwa namung’unya ubuyu mdomoni, alichokifanya aliniambia nizimeze zile mbegu za ubuyu, sikuwa na namna ilibidi nifanye hivyo japo ilikuwa ngumu kumeza.
“Kama nilivyosema awali mimi sikuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na msichana yeyote kuanzia shule ya msingi mpaka namaliza kidato cha nne ila shuleni nilikuwa na bahati ya kuwa kiongozi wa darasa (kiranja), basi kuna siku niliviziwa na huyo Afande Miraji akanikuta niko mbele nazungumza kwa kelele za juu na kulifanya darasa zima lisiwe na utulivu. Hivyo Miraji akanipa adhabu nyingine ya kuchimba shimo. Nakumbuka adhabu hiyo ilinifanya mwili wangu uchoke siku nzima ndiyo maana hadi leo pamoja na utundu wangu wote niliopitia hapo nyuma, Miraji kwangu alikuwa ni kiboko, kifupi alinifanya niwe ngangari.
“Kitu kingine ambacho ni moja ya vitu ambavyo sitavisahau ni pamoja na kulipenda sana somo la historia kwa sababu tu ya Military Police (MP) ambaye alikuwa…
Simulizi hii itaendelea wiki ijayo ni vyema uifuatilie mpaka mwisho ili upate kujua mambo mengi yaliyojiri na yanayoendelea kutokea katika maisha ya Mkwere ambayo naamini yatakupa darasa katika maisha yako kuhusiana na kutokata tamaa au kukifanyia kazi kipaji ulichojaliwa na Mwenyezi Mungu kama yeye ambapo kipaji chake kimegeuka kuwa ajira inayomuingizia kipato.

Note: Only a member of this blog may post a comment.