Tuesday, March 29, 2016

Anonymous

Mashabiki Waleta Fujo Ukumbini Kisa, BELLA

Christian Bella ‘Obama’ amefunguka mambo mengi sana kwenye simulizi hii ya maisha yake. Alielezea jinsi alivyoacha shule kutokana na baba yake zazi kufukuzwa kazi, alivyolazimika kuhama nyumbani kwao Kongo na kuingia mtaani kupigania ndoto zake, lakini kubwa zaidi alivyokazania kile alichoamini kingemkomboa katika maisha yake.
Si hayo tu, mengi sana amefungukia na wiki iliyopita alielezea namna alivyojikuta katika mgogoro na Totoo Ze Bingwa lakini pia alielezea namna alivyokuwa anachukizwa kwa kufananishwa na Fally Ipupa.
Tambaa naye…

BELLA anaendelea kufunguka kuwa si kwamba alikuwa anachukia kufananishwa na Fally Ipupa, ambaye ana mafanikio makubwa kimuziki kwa sababu hakuwa anazikubali kazi zake.
Anakiri kumkubali na anamtaja kuwa miongoni mwa ‘maroll model’ wake lakini hata hivyo kwa sasa Bella anasema anafikiri yeye ni bora kuliko Fally na wasanii wengine wengi kutokana na uwezo wake kukua na sauti yake kuwa ya pekee ambayo si rahisi kuifananisha na msanii mwingine.

“Unajua watu huwa wanashindwa kumuelewa Bella. Huwezi kunifananisha mimi na msanii yeyote yule kwa sababu sauti yangu ni ya dhahabu, ninajivunia hilo na ninafikiri kati ya vitu ambavyo Mungu amenibariki na kunitofautisha na watu wengine ndiyo hicho pekee, kwa hiyo nilikuwa sifurahii kabisa kufananishwa na Fally Ipupa,” anasema Bella.
Anaendelea kuwa suala hilo aliamua kuliweka wazi mara kwa mara alipokuwa kwenye mahojiano na vyombo vya habari na taratibu anafkiri watu waliendelea kumuelewa maana hali hiyo ilifikia hatua ikakata.

Bella anaendelea kuwa suala lingine ambalo hata kuja kulisahau lililomtokea kwenye kazi yake ya muziki kiasi cha kuhatarisha kumvunjia heshima na kumpotezea mashabiki wengi ni varangati lililoibuka mwishoni mwa mwaka 2014, katika Ukumbi wa White House uliopo Korogwe jijini Dar es Salaam!
Anasema ishu nzima kulikuwa na tamasha limeandaliwa na katika tamasha hilo kati ya wasanii waliokuwa wanatarajiwa kufanya onesho yeye pia jina lake lilikuwa miongoni mwao.

Lakini hata hivyo katika hali ya kushangaza hakuwa na taarifa hizo na wala hakuwepo nchini.
Sasa siku ya tamasha ilipowadia, mashabiki walifurika wakitegemea mmoja wa waburudishaji alikuwa ni yeye na bendi yake jambo lililosababisha fujo kubwa baadaye baada ya wasanii wote kutumbuiza bila yeye kuonekana.

“Nilizipata taarifa hizo kutoka kwa watu wangu wa karibu kuwa raia walianza kuvunja viti na chupa hovyo huku wakipiga kelele kwa kulitaja jina langu,” anasema Bella na kuendelea kuwa;
Baada ya kuzisikia taarifa za sakata hilo aliporudi Bongo, alikwenda moja kwa moja kuonana na waandaaji wa tamasha hilo ili kuhoji ni kwa nini waliamua kulitumia jina lake bila kuwasiliana naye.

Anasema waandaaji hao hawakuwa na jibu la kumpa zaidi ya kumuomba radhi na kumtaka walimalize suala hilo kibinadamu, hicho ndicho kilichotokea, baada ya maelewano kila kitu kiliishia pale na mambo mengine yakasonga mbele.

Bella anasema mpaka hapa alipofikia leo kimafanikio katika kazi zake za kimuziki ni mapenzi ya Mungu na juhudi ambazo amekuwa nazo tangu mwanzo na haitatokea hata siku moja akarudi nyuma.

Anaendelea kuwa kwa watu wanaotamani kufanikiwa hasa kwa kutimiza ndoto walizonazo ni muhimu kujitoa kwa asilimia mia moja katika kile wanachokiamini lakini zaidi ni kujifunza nini kinahitajika wafanye ili kuwarahisishia safari yao.
“Wapo watu wengi wanapenda kufanikiwa, lakini hawafahamu nini wafanye ili kufikia mafanikio yao. Napenda kuwapa moyo kuwa katika safari ya mafanikio hakuna miujiza yoyote bali ni juhudi na nia ya dhati ya mhusika mwenyewe.
MWISHO.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.