Wednesday, March 9, 2016

Anonymous

Beki AZAM FC Ataka Mkataba YANGA SC

SONY DSC
BEKI wa kati wa Azam FC, Said Morad.
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BEKI wa kati wa Azam FC, Said Morad amesema anaelekea kumaliza mkataba wake na timu hiyo na yupo tayari kujiunga na timu yoyote ya Ligi Kuu Bara lakini chaguo lake la kwanza ni Simba au Yanga.
Mkataba wa mwaka mmoja wa Morad na Azam unamalizika Mei 30, mwaka huu na hadi sasa hajaambiwa lolote kuhusu mkataba mpya hivyo ameanza kujiweka sokoni ili asikose timu msimu ujao wa ligi kuu.

Rafiki wa karibu wa mchezaji huyo aliliambia Championi Jumatano jana Jumanne kwamba, mkataba wa mchezaji huyo unaelekea ukingoni bila ya kuambiwa lolote na uongozi wa Azam na hivyo anaona bora asepe zake.
“Mkataba wake na Azam unaisha Mei 30, mwaka huu, hajaambiwa lolote hadi sasa ndiyo maana anasema yupo tayari kwenda popote penye maslahi, hata iwe Simba au Yanga.

“Amesema atafurahi zaidi akienda Yanga kuongeza ulinzi wa kati na Yondani (Kelvin) ila itategemea zaidi na atakachoambiwa na Azam maana ndiyo timu yake ya sasa,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, Championi lilimtafuta Morad ambaye alisema kuwa ni kweli mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu na yupo tayari kwenda popote.

“Mkataba wangu unamalizika mwishoni mwa msimu huu, nipo tayari mimi kwenda popote lakini lazima iwe timu kubwa kama Simba au Yanga, lakini kwa sasa mimi bado ni mali ya Azam na wakizungumza nami nitawapa kipaumbele,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Ashanti United, Simba na Kagera Sugar.

Katika kikosi cha Azam, Morad amekuwa akicheza beki ya kati sambamba na Pascal Wawa na David Mwantika katika mfumo wa 3-5-2 ambao huchezwa na mabeki watatu wa kati.
Wikiendi iliyopita alishirikiana vyema na wenzake kuwazuia washambuliaji wa Yanga wakiwemo Amissi Tambwe na Donald Ngoma na kulazimisha sare ya mabao 2-2.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.