Mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe.
Said Ally, Dar es SalaamBAADA ya kufungua akaunti yake ya mabao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe, ametamka kuwa ndoto zake ni kuona anafikia rekodi ya Mtanzania, Mbwana Samatta ya kuhakikisha anatwaa tuzo ya ufungaji bora wa michuano hiyo.
Tambwe amefanikiwa kufunga bao moja kwenye michuano hiyo dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius ambapo ameanza safari ya kusaka tuzo ya kutwaa kiatu hicho ambacho kinashikiliwa na Samatta baada ya kutwaa msimu uliopita alipofunga mabao nane.
Tambwe mwenye mabao 15 katika ligi, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, ndoto yake kubwa ni kuona anafikia rekodi hiyo ya Samatta ya kuibuka mfungaji bora wa Afrika ambapo itamuongezea sifa katika kuonekana kimataifa kwani amepanga kuyatumia mashindano haya kama sehemu mojawapo ya kujitangaza.
“Lakini kingine nimepanga kuitumia michuano hii ya kimataifa katika kukuza soko langu la kujitangaza kimataifa kwani kama unavyojua mashindano haya yanafuatiliwa sehemu kubwa ya Afrika, hivyo kama nitafanya vyema naweza nikapata ofa nzuri katika klabu nyingine ndani au nje ya bara hili,” alisema Tambwe.

Note: Only a member of this blog may post a comment.