Tuesday, August 11, 2015

Anonymous

DK. MAGUFULI Ana Kila Sababu ya Kuingia Ikulu

magufuliMgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa John Pombe Magufuli.
Gumzo kubwa kwa sasa nchini Tanzania, ni juu ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa John Pombe Magufuli!
Tayari Magufuli ameshachukua fomu ya kugombea urais sambamba na wagombea wa vyama vingine lakini kwa jinsi upepo wa kisiasa ulivyo, inaonesha itakuwa rahisi zaidi kwake kuingia ikulu kuliko mgombea mwingine yeyote kutokana na sifa alizonazo. 

Mchakato wa kumpata mgombea mmoja kati ya 38 waliokuwa wanawania nafasi ya kuteuliwa na CCM kushika nafasi hiyo, haukuwa mwepesi hata kidogo. Sote tutakumbuka jinsi makada wengi wakubwa walivyokuwa wakipigana vikumbo mjini Dodoma.
Mwisho, nyota ya jaha ikamuwakia Magufuli ambapo mkutano wa chama hicho, ulimchagua kwa kishindo kuipeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Magufuliii (5)-001Zipo sifa nyingi ambazo ndiyo hasa zilizomfanya Magufuli awabwage makada wenzake wa chama hicho na sifa hizohizo ndiyo zitakazowafanya Watanzania wamchague kuingia ikulu kwenye uchaguzi mkuu. 

Tofauti na makada wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo ndani ya CCM, Magufuli hakuwa na kashfa wala skendo hata moja, sifa ambayo kwa sasa ni nadra kuikuta kwa viongozi wa nchi hii. Magufuli hajawahi kuhusishwa na kashfa yoyote ya matumizi mabaya ya madaraka wala rushwa! CV yake ni safi kabisa katika kipengele hicho. 

Tanzania ya leo inahitaji kiongozi ambaye si mla rushwa, mroho wa madaraka wala anayeendekeza vitendo vilivyo kinyume na maadili ya uongozi na sheria za nchi. Endapo Watanzania watazingatia kigezo hicho, Magufuli atapeta kwa kishindo!
Magufuliii (4)-001
Ndiyo, Watanzania wanategemea mtu atakayewavusha katika ‘bahari ya ufisadi’ kuelekea ‘nchi ya ahadi’ asiwe na madoa yanayohusu ufisadi wala matumizi mabaya ya madaraka. Magufuli ni msafi tofauti na wagombea wengine wa nafasi hiyo kutoka vyama vingine.

Ukija katika suala la uchapakazi, sote ni mashahidi wa jinsi alivyoziongoza vyema wizara zote alizowahi kuzitumikia sambamba na wananchi wake wa Chato.

Sote tumeshuhudia barabara nyingi ambazo kipindi cha nyuma zilikuwa hazipitiki katika majira yote ya mwaka hasa masika, zikijengwa kwa kiwango cha lami na kuwakwamua Watanzania wengi.

Pia amejitahidi kujenga madaraja yanayopitika majira yote ya mwaka sehemu mbalimbali za nchi hii. Ukijaribu kupima utendaji kazi wa mawaziri wengi, utagundua kwamba Magufuli anaweza kuwa anaongoza kwa kukamilisha miradi mingi chini ya wizara yake.

Kama Watanzania watataka kumchagua rais mchapakazi, asiye na hata chembe ya ubabaishaji, Magufuli pia atapeta.

Suala jingine linaloweza kuwa karata dume kwa Magufuli kuingia ikulu, ni uwajibikaji wake. Magufuli si kiongozi wa kukaa ofisini kama walivyo watendaji wengi wa serikali. Mara kwa mara tumekuwa tukimshuhudia akitembelea mwenyewe miradi mbalimbali chini ya wizara yake, wakati mwingine hata nyakati za usiku.

Magufuli si mtu wa kusubiri kuletewa ripoti bali huongoza kwa vitendo. Mara kadhaa amewatoa nishai wakandarasi wababaishaji ambao huidanganya serikali kwamba wamejenga miradi mbalimbali kwa kiwango kinachotakiwa kumbe nyuma ya pazia hufanya usanii.

“Mzee huwa anakwenda mwenyewe kukagua miradi, wakati mwingine bila hata kutoa taarifa, ghafla mnashtukia tu mheshimiwa huyo! Hata kama mlikuwa mnachakachua, ni lazima atawabamba kwa sababu anakuja bila taarifa, tunahitaji kiongozi wa namna hii,” Herman Massawe, mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam alimwambia mwandishi wa makala haya katika mahojiano ya kawaida.

Pamoja na sifa binafsi, Magufuli pia anabebwa na sifa ya chama chake kwa sababu ipo wazi kwamba CCM ndiyo chama pekee Tanzania kilichosambaa mpaka ngazi ya vijijini kabisa na kwenye maeneo mengine ambayo vyama vingine vya siasa havijafika.

Kwa msingi huo, endapo Watanzania wote watajitokeza na kupiga kura, hasa wale wa vijijini, ni dhahiri Magufuli atapata kura nyingi kuliko mgombea mwingine yeyote na hivyo kumrahisishia safari yake ya kuelekea ikulu na kuwatumikia Watanzania.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.