Straika wa Stand United, Elias Maguri.
Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam.
LICHA ya kuachwa kwa mabao sita na kinara wa mabao Ligi Kuu
Bara, Hamis Kiiza wa Simba, straika wa Stand United, Elias Maguri,
hajakata tamaa na bado anakiota kiatu cha dhahabu.
Kiiza ana mabao 16 akifuatiwa na Amissi Tambwe wa Yanga aliyefunga
mabao 15 huku Jeremiah Juma wa Prisons na Donald Ngoma wa Yanga wakiwa
na mabao 11 kila mmoja. Maguri ana mabao 10.
Amissi Tambwe wa Yanga akishangilia na wachezaji wenzake.
Tangu kuingia mwaka huu, Maguri amefunga bao moja tu wikiendi
iliyopita dhidi ya JKT Ruvu na kuiwezesha timu yake kutoka sare ya bao
1-1 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Maguri ambaye
alikuwa akiwekwa benchi na kocha wake Patrick Liewig kwa maelezo ya
kujiona staa, alisema anaamini ndani ya mechi sita atakuwa anaongoza kwa
mabao.
Hamis Kiiza wa Simba.
“Nimeanza kucheza sasa, namuomba Mungu anipe afya njema niendelee na
kasi yangu ya ufungaji niweze kuwaacha Tambwe na Kiiza ambao waliniacha
baada ya kupata matatizo na kocha.
“Najua haitakuwa kazi nyepesi lakini nitapambana vilivyo kuhakikisha
nawaacha na ikiwezekana mpango huo uweze kutimia ndani ya mechi zetu
sita za ligi,” alisema Maguri aliyewahi kucheza Simba.

Note: Only a member of this blog may post a comment.