Beki wa kati wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ .
Wilbert Molandi, Dar es SalaamNDIYO kwanza amerejea uwanjani akitoka kuuguza jeraha la enka, lakini nahodha na beki wa kati wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema anahitaji siku saba tu za kuwa fiti tayari kuivaa Simba.
Beki huyo, alianza mazoezi ya pamoja na wenzake, Jumanne iliyopita jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza programu ya mazoezi binafsi. Cannavaro alikuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi miwili.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Cannavaro alisema mazoezi anayofanya hivi sasa ni kukimbia mbio ndefu na fupi pekee kabla ya kucheza mpira pamoja na wenzake.
“Nimeanza mazoezi wiki hii bado sijawa fiti kwa asilimia kubwa kwa maana ya kufanya mazoezi ya nguvu ikiwemo kucheza mpira kabisa.
“Nitakuwa na programu kwa siku saba pekee nitakayoimaliza kabla ya mechi ya Simba na kuanza mazoezi nikiwa fiti kwa ajili ya mchezo huo,” alisema Cannavaro ambaye yupo Mauritius na Yanga ambayo leo inacheza na Cercle de Joachim katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Note: Only a member of this blog may post a comment.