Sunday, November 15, 2015

Anonymous

UVCCM Yazidi Kumkaba Maalim Seif Sharif Hamad...Yawatoa Hofu Vijana wa Zanzibar

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umewataka vijana Zanzibar kutobabaishwa na kuendelea kwa mjadala au mazungumzo ya viongozi wa kisiasa kuhusu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu ambao umefutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

UVCCM imesema mazungumzo hayo ni sehemu ya harakati za kuhakikisha amani inaendelea kuwepo nchini na kwamba hayawezi kubadilisha uamuzi wa ZEC katika uchaguzi huo.

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema hayo jana katika mkutano wake na wajumbe wa umoja huo na viongozi wengine wa CCM ngazi za kata, majimbo na wilaya kwenye ukumbi wa CCM Dimani, katika Mkoa wa Magharibi Unguja.

Alisema Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ni mchakato unaosimamiwa na Sheria ya Uchaguzi, hivyo hakuna yeyote mwenye mamlaka wala madaraka ya kuiingilia ZEC, kuipangia au kulazimisha ipindishe sheria kwa maslahi ya wachache.

“Kukaa kwetu kimya haimaanishi kwamba sisi si weledi wa kusema na kujipamba kwa sifa na majigambo yasiyo na maana katika jamii, tunataka tutofautishwe kati ya wanaojua na kuheshimu nguvu ya sheria na wale wanaoropoka hovyo bila kujali maslahi ya nchi,” alisema.

Katibu Mkuu huyo aliwaeleza wanachama hao wa CCM kwamba, tangu ZEC itangaze kufuta matokeo ya uchaguzi huo, kumekuwa na kauli mbalimbali za kibabaishaji kutoka kwa baadhi ya viongozi wa upinzani, akiwemo Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
“Hatushindwi kumjibu Maalim Seif, chama chake na wote wanaomuunga mkono, tunachelea kuonekana mbumbumbu mbele ya waelevu,” alisema Shaka. 
 
Alisema sheria inampa mamlaka Mwenyekiti wa ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi kama alivyofanya baada ya kugundua kukiukwa kwa taratibu.

Kwa mujibu wa Shaka, baada ya uamuzi huo anaepita mitaani na kusema anasubiri aapishwe awe Rais wa Zazibar wakati Ikulu ipo chini ya rais halali kisheria, huyo anaota mchana na anajiweka wazi jinsi alivyo na uchu wa madaraka.

Aidha, alisema mivutano itokanayo na utata wa kisheria haitamalizwa na vinywa vya wanasiasa wenye tabia ya kukanyaga sheria au kubeza matakwa ya katiba. Kwa mujibu wa shaka, sehemu yoyote inayohitaji msaada wa mazungumzo, ni jambo la kawaida kwa wanasiasa na viongozi kukutana, ingawa hatua hiyo haihalalishi kuvunjwa kwa sheria na katiba ya nchi.

Shaka alisema uendeshaji wa nchi yoyote duniani, husimamiwa na kulindwa kisheria na katiba, hivyo kinaweza kuwa kituko iwapo mwanasiasa atadhani kwa kushinikiza jambo, anaweza kupewa nafasi ya uongozi wa juu wa nchi.

“Iwapo ZEC imefuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu kutokana na uwezo wa kisheria walionao, sasa ni wajibu wao tena kuwaeleza wananchi ni lini watapiga kura tena, ili watimize haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa kidemokrasia,” alisisitiza.

Aliwataka vijana wa CCM kuwa makini, wavumilivu na wenye ari ya kudumisha mapinduzi yao, huku akiwataka kusahau wale wote wenye mawazo ya kutaka kuyazika kwa kuwa hilo halitawezekana milele.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.