Na Haruni Sanchawa
TENA! Kifo cha
aliyekuwa Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher
Mtikila (pichani) aliyefariki dunia Oktoba 4, mwaka huu kimetikisa upya
baada ya naibu katibu mkuu wa chama hicho, Abdul Juma kutoa mwezi mmoja
kwa polisi iwe imetoa majibu ya uchunguzi wake.
Akizungumza na gazeti hili juzi jijini
Dar, katibu huyo alisema licha ya Oktoba 22, mwaka huu mke wa marehemu
Mtikila, Georgia Mtikila kulalamikia mazingira ya kifo cha mumewe,
polisi hawajatoa taarifa yoyote juu ya uchunguzi wao.
Alisema kifo cha Mtikila kilikuwa cha
kutatanisha ndiyo maana mama Mtikila alimuomba rais aliyemaliza muda
wake, Jakaya Kikwete kuunda tume ya uchunguzi kwani wote waliopata ajali
na kiongozi huyo, mpaka sasa hawajulikani walipo na hakuna hata mtu
mmoja anayeshikiliwa.
Akaongeza: “DP ilikuwa na imani kubwa na
Kikwete kwamba angeunda tume ya uchunguzi kwa vile aliyefariki dunia ni
mwenyekiti wa kitaifa wa chama halali cha siasa ambaye alikuwa na
mchango mkubwa katika nchi.
“Hata hivyo, DP na familia ya Mtikila
ina imani kubwa kwamba, Rais John Pombe Magufuli ataliona hili kwa vile
amepokea kijiti cha uongozi kutoka kwa Kikwete.”
Hata hivyo, aliongeza kwamba licha ya
kuwa na imani na Magufuli, wanatoa mwezi mmoja, wakiona kimya watafanya
kila mbinu ya kumuona kiongozi huyo mpya wa nchi ili ufumbuzi upatikane.

Note: Only a member of this blog may post a comment.